Stars yalazimishwa sare

Timu ya soka ya taifa, Taifa Stars.

Timu ya soka ya taifa, Taifa Stars jana ililazimishwa sare ya bao 1-1 na wenyeji wao, timu ya taifa ya Yemen katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa ambao ulifanyika nchini humo kuanzia saa 10 kamili jioni sawa na saa hapa nyumbani.

Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, Stars na Yemen kila mmoja ilishindwa kumtambia mwenzake baada ya kumaliza dakika 45 za kwanza wakiwa hawajafungana.

Stars ambayo Alhamisi iliyopita ilikubali kipigo cha bao 5-1 kutoka kwa mabingwa wa zamani wa Afrika, timu ya taifa ya Misri ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao katika dakika ya 69 kupitia kwa mshambuliaji wake, John Bocco.

Hata hivyo Stars ambayo inatumia mechi hizo kujiandaa na mashindano ya Chalenji ya nchi za Afrika Mashariki na Kati yaliyopangwa kuanza kufanyika mwishoni mwa mwezi huu ilishindwa kulinda bao hilo na kuruhusu Yemen kusawazisha baada ya dakika 10.

Katika mechi ya jana, langoni mwa Stars alikuwa kipa, Shabani Dihile ambaye ndiye kipa namba moja wa timu hiyo hivi sasa tangu alipoachwa Ivo Mapunda.

Stars na wenyeji hao wanatarajia kucheza mechi nyingine ya marudiano hapo keshokutwa na kurejea nyumbani.

Katika orodha ya viwango ya Shirikisho la soka duniani (FIFA), Tanzania iko katika nafasi ya 99 wakati Yemen ni ya 139.

Misri ambayo wameamsha ‘hasira’ za watanzania kwa mara nyingine kwa kutaka kocha mkuu wa Stars, Mbrazil, Marcio Maximo atimuliwe baada ya kuipa kichapo timu yao yenyewe iko katika nafasi ya 28 katika orodha ya FIFA.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments