KWA HILI MADEGA ALIKUWA SAHIHI

Na Ibrahim Mkamba

NINAPENDA  kumuunga mkono Mwenyekiti wa Yanga,Imani Madega kwa hatua sahihi aliyochukua kiuongozi kuiokoa timu yake isipate kashfa na kupoteza pointi mezani kwenye mechi yake ya kwanza ya ligi kuu msimu huu dhidi ya timu ya African Lyon ya Dar es Salaam. Ninashangaa kuona wenzangu wengi wakimpiga madongo mazito kiongozi huyo kwamba hakuwa sahihi kuchukua hatua hiyo.Kabla sijaingia ndani ya suala husika,naomba leo nianze na katuni moja ya Godfrey Mwampembwa ya Bi Mkora.

Katika katuni hiyo,malaika alionekana juu ya wingu akiwa na mhusika mjinga mjinga katika katuni ya Bi Mkora anayeitwa Pampula.Malaika alisema kwa mtu ambaye hakuonekana kwenye mchoro huo kumuomba  ampokee mwanadamu huyo na kumtunza mahali pazuri kwa sababu alikuwa mwadilifu mno.Aliueleza uadilifu wake kwamba alitumwa kwenda nchi za mbali kutafuta maji kwani nchini kwao hakukuwa na maji.Malaika aliendelea kueleza kuwa alipoyapata maji hayo alisafiri nayo kama yalivyo.Hakudokoa hata kidogo, hata aliposhikwa na kiu kali, ili ayafikishe yote kama yalivyo naye apate mgao sawa kama wengine baada ya kuyafikisha.

Malaika wa katuni ya Mwampembwa aliendelea kueleza kuwa kutokana na uadilifu wa mwanadamu huyo ( Pampula),aliyafikisha maji hayo kwa wenzake lakini mwenyewe alikufa kwa kiu iliyosababishwa na yeye kuwa mwadilifu kwa kutokunywa sehemu ndogo ya maji hayo kukata kiu yake! Kwa hiyo Malaika aliomba mwanadamu huyo apokewe kwa heshima.Baada ya ombi hilo,sauti kutoka upande wa juu wa mchoro huo ilijibu kwa kusema kuwa mwanadamu huyo asingepokewa huko  kwani huko hawapokewi wanadamu wajinga! Tafsiri ni kwamba kitendo cha Pampula kufa kwa kiu wakati alikuwa na maji mengi mkononi au kichwani,ulikuwa si uadilifu bali ujinga. Ni kweli, ni ujinga.Mtu unaona kuna hatari ya wazi kabisa,huchukui hatua eti kwa sababu ya kuogopa kuonekana utakuwa umekiuka taratibu fulani,ni ujinga.Usalama wakati wowote ni kitu cha kwanza,mengine yanafuata.

Wakati wa mechi ya Yanga na African Lyon ambayo ilikuwa moja ya mechi za ufunguzi wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu,kocha Dusan Kondic aliandaa wachezaji wa nje saba kuhusika na mechi hiyo badala ya watano wanaokubalika kikanuni.Hilo lilikuwa kosa ambalo lingeyagharimu vibaya sana maisha ya Yanga kwenye matokeo ya mechi hiyo kama kiu ilivyoyagharimu maisha ya Pampula kwenye katuni ya Mwampembwa niliyoikumbuka.Wadau wa soka waliomlaumu Madega kwa hatua aliyochukua kuweka sawa mambo ili Yanga isipoteze ushindi mezani wananipa mashaka makubwa kama wao ni watenda haki.

Kuna waliodai kuwa hadithi ya Madega haikuwa ya kweli bali aliitunga hadithi hiyo kujitetea dhidi ya kitendo chake cha kumuingilia kocha.Kuna walioenda mbali zaidi na kudai kuwa Kondic asingeweza kufanya ujinga huo kwani siku zote,kwa nafasi yake,anajua kila kitu kuhusu masuala ya ufundi yakiwemo kanuni, kadi za wachezaji wake,adhabu za wachezaji wake na kadhalika na baadhi walihoji kama viongozi wa klabu hiyo walishamkumbusha kocha huyo kuhusu matatizo ya kikanuni yaliyohusu wachezaji yaliyotangulia kabla ya hili.

Nina hoja mbili za kupingana na wadau hao.Kwanza,kauli ya Kondic aliyoitoa kwa hiari yake huku akiwa na akili timamu kwamba hakujua idadi ya wachezaji wa nje wa kutumika kwa mechi na kulaumu kwa kutojulishwa hilo mapema inafutilia mbali  madai kwamba hadithi ya Madega ilikuwa hadithi ya kutunga.Cha ajabu ni kwamba waliomlaumu hivyo Mwenyekiti huyo wa Yanga na timu yake ya uongozi walifanya hivyo baada ya kuzisikia kauli zote tatu, ya Kondic ya kudai kuingiliwa,ya Madega ya kuiokoa timu isipoteze pointi mezani na ya Kondic ya  kutenda kweli kosa la kupanga wachezaji wa nje saba kwa sababu alikuwa hajajulishwa na viongozi wake kanuni hiyo.

Hapa sioni kina Madega wamekosea nini  na kuitwa kuwa watu waliomuingilia kocha wakati kocha mwenyewe amewalaumu kwa kutomuelimisha mapema kuhusu kanuni ya idadi ya wachezaji wa nje kwa mechi.Kama huko kukumbushana tunakuita kuingilia kazi ya kocha,basi hata kocha mwenyewe alikuwa tayari kuingiliwa kazi yake lakini alitaka afanyiwe hivyo mapema na si siku ya mechi akiwa ameshaandaa wachezaji wa nje saba kushiriki mechi ya timu yake na African Lyon.

Kuhusu la pili,sishangai  viongozi wa Yanga kutokumbusha lolote kabla kwa dawati lao la ufundi. Wangekumbusha nini kama  kila kitu kilikuwa sawa? Kama mambo yangekwenda ndivyo sivyo, ni wazi wangeweka sawa kama inavyothibitishwa na walivyofanya kwenye tukio hili la wachezaji wa kigeni saba.

Naomba tuwekane sawa kidogo.Hakuna mamlaka yoyote duniani isiyokaguliwa hata kama mamlaka hiyo ni huru kwa kiasi gani.Utaratibu huo ndiyo unaoleta msingi wa “Checks and Balances” (Ukaguzi wa matumizi ya mamlaka na uwianisho wa nguvu za kimamlaka).Katika msingi huo,uongozi wa klabu unawajibu wa kuingilia shughuli za dawati la ufundi la klabu kama uongozi huo unaona kwamba kutofanya hivyo kuna athari kwa klabu.Moja ya athari hizo ni kupoteza pointi mezani kizembe.Huu ndiyo uongozi makini.Hivi tulitaka nani amsahihishe Kondic kama si viongozi wa klabu.Na kama shabiki yoyote angefanya hivyo,kwanza,nguvu gani ya shabiki huyo ingemlazimisha kocha arekebishe kosa lake na pili shabiki huyo angepata wapi uhalali wa “kumuingilia kocha” ambao hata viongozi wa klabu hawana? Tofauti na mashabiki,viongozi wana nguvu ya kiuongozi ya kumuelekeza kocha jambo jema naye akatekeleza.

Kondic alikuwa hajui idadi ya wachezaji wa nje wa kutumika kwa mechi moja au alitaka kufanya makusudi tu kuwatumia akikusudia matokeo anayoyajua mwenyewe.Uongozi wa Yanga umeona kosa hilo.Kwa nini tulitaka uongozi huo unyamaze tu na Yanga iharibikiwe? Kama mambo yangeharibika baada ya viongozi wa Yanga “kutomuingilia” kocha na kumkumbusha idadi ya wachezaji wa nje aliopaswa kuwatumia kwa mechi,sisi hawa hawa tungewajia juu viongozi hao na kuwaita majina mengi mabaya mabaya kama wazembe,wasiowajibika,wasio watu wa soka,wabababishaji na kadhalika hasa baada ya kocha kusema kuwa alipanga idadi hiyo baada ya viongozi kutomjulisha kuhusu kanuni hiyo.

Ni vizuri tukumbushane kwamba Madega,kama kiongozi mkuu wa Yanga, anaongoza shughuli zote za klabu hiyo,ikiwemo timu ya soka.Haiingii akilini kumtaka asimamie maendeleo ya timu huku tukimtaka asijue lolote kuhusu timu hiyo wakati mahitaji ya timu hiyo yanawasilishwa kwake na huku taarifa ya maendeleo ya kambi ikiwasilishwa kwake! Kwa nini hatutaki yeye kujua tu kwamba leo watacheza vijana wake kina nani? Nalisema hili kwa sababu baadhi yetu tulifikia hatua ya kuhoji Madega alijuaje kama Kondic alipanga wageni saba siku hiyo kama si kuomba orodha ya wachezaji waliopangwa siku hiyo.Kwa nini Madega asijue wakati tulio nje ya klabu tunaweza kujua kupitia vyombo vya habari ambavyo viko huru kupewa orodha hiyo? Vyombo vya habari vipewe na si Mwenyekiti wa klabu,mwenye timu!

Wachambuzi wengi wa soka kwa sasa tumefanya kama “fasheni” kuwasema sana viongozi wa klabu zetu za soka hasa wa Yanga na Simba.Maandishi yetu yatakuwa na thamani kama tukifanya hivyo katika kuwaweka kwenye mstari sahihi.Kinyume chake,tutajidharaulisha vibaya sana tukiwasema vibaya hata pale wanapostahili pongezi kama  Madega alivyostahili pongezi  kwa uamuzi mzuri alioufanya alipoiokoa timu yake kutoka kwenye fadhaa,kashfa na hasara. Kwa upande mwingine, kama aliye kituko cha soka katika suala lolote ni kocha,maandishi yetu yajielekeze katika kumshangaa kocha huyo kama Kondic asiyejua kanuni ya ligi inayotumika kwa msimu wa tatu sasa badala ya kupindisha ukweli wa mambo na kuwalaumu viongozi kwa wasilostahili lawama!

Ni vizuri tukijikumbusha kwamba aliyekuwa kocha wa Simba Jamhuri Kihwelo alipompanga Juma Nyosso aliyefungiwa,uongozi wa klabu ungemzuia,Simba isingepata hasara ya kunyang’anywa pointi mpaka kukosa nafasi ya pili kwenye msimu wa ligi wa 2007/08.Je huko “kutomuingilia kocha” kwa viongozi wa Simba kuliipa faida gani klabu hiyo?

Ninavyoona, tatizo baya sana la viongozi wa klabu zetu kuingilia upangaji wa timu au kupanga timu linahitaji mjadala tofauti lakini hili la Madega kurekebisha kosa la kuigharimu timu yake linapaswa lijadiliwe ki tofauti kwa sababu ni masuala yaliyo tofauti sana.Kama mwanadamu wa katuni ya Mwampembwa alikataliwa kupokewa sehemu ya raha kwa sababu alikuwa mjinga kwa kutojali usalama wake ili aonekane  mwaminifu, ndivyo ambavyo Madega leo hii asingeishi kwa raha,endapo Yanga ingepoteza pointi moja (kama matokeo yangekuwa kama yalivyokuwa) kutokana na kiongozi huyo kutojali usalama wa timu yake ili asionekane anamuingilia kocha!

Katika utendaji wetu mahali popote pale,usalama unatangulia mambo yote na ndiyo maana nasema kwa hili, Madega alikuwa sahihi na anastahili pongezi nyingi.Naomba wengine waige toka kwa mwenzao kuchukua hatua kama hii kila inapobidi na kwa kufanya hivyo wala watakuwa hawawaingilii makocha bali watakuwa wanajali maslahi ya timu zao na kulinda pia mafanikio ya hao hao makocha.Nawatakia heri viongozi wa klabu zote za ligi kuu katika kusimamia kwa usahihi ushiriki wa timu zao katika ligi hii ngumu.Vyovyote itakavyokuwa,usalama kwanza.

ibrahim Mkamba [email protected]

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments