Yanga yazinduka, Simba yapaa Ligi Kuu ya Vodacom.

Moja katika ya matukio wakati klabu za Simba na Manyema zote za Dar es Salaam zilipopambana na Simba kuifunga Manyema 2-0.

SIMBA na Yanga zimevuna pointi tatu muhimu katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom zilizochezwa kwenye viwanja vya Uhuru Dar es Salaam na Jamhuri, Morogoro.

Simba iliinyamazisha Manyema ‘Mkuki wa Sumu’ kwa kuifunga mabao 2-0 ya mikwaju ya penalti katika mchezo uliotawaliwa na ubabe wa wachezaji wa pande zote mbili.

Yanga ambao walishuhudiwa na mfadhili wao, Yussuf Manji aliyeingia Jamhuri kwa gari aina ya Range Rover, rangi nyeusi iliondoka na ushindi huo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Matokeo hayo yanaifanya Yanga kufikisha pointi nane baada ya mechi tano wakati Simba imefikisha pointi 15 na kuweka rekodi ya kushinda mechi zote tano.

Katika mchezo wa jana, Yanga iliingia Morogoro ikiwa imekamilika ikiongozwa na Manji, mwenyekiti wao, Imani Madega huku kocha wa timu hiyo, Dusan Kondic akiwashuhudia vijana wake kutoka jukwaani.

Kocha msaidizi, Spaso Sokolovsk na Kenny Mkapa ambaye ni meneja wakikalia benchi la ufundi la timu hiyo.

Ukiacha hayo, mchezo ulianza taratibu, lakini kwa kukamiana huku Yanga ikitawala sehemu ya kiungo katika uwanja uliokuwa umejaa vumbi kutokana na kutomwagiwa maji.

Katika dakika ya 22, nusura wapate bao baada ya Abdi Kassim kuachia shuti lililotemwa na kipa Shaaban Kado, lakini Moses Odhiambo aliuwahi na kuachia shuti ambalo lilipaa na kutoka nje.

Katika kipindi cha kwanza, Mtibwa Sugar ilifanya mashambulizi mengi, lakini hata hivyo, washambuliaji wake hawakuwa makini.

Pamoja na mashambulizi hayo, kikwazo kikubwa kilikuwa ngome ya Yanga iliyokuwa chini ya George Owino na Wisdom Ndhlovu kama ilivyo kwa Mtibwa Sugar chini ya Idrisa Rajab, Obadia Mungusa na Chacha Marwa.

Dakika 54, kiungo Nurdin Bakari aliipatia Yanga bao la kuongoza kwa shuti kali la adhabu ndogo kutokana na mabeki wa Mtibwa kutojipanga vizuri.

Dakika nne baadaye, Mrisho Ngassa alifumania nyavu kwa mpira wa kichwa na kuifanya Yanga kufikisha pointi nane.

Bao la kufutia machozi la Mtibwa Sugar liliwekwa kimiani na Soud Abdi katika dakika ya 64. Hata hivyo, Yusuf Mgwao alifunga katika dakika ya 82, lakini lilikataliwa na mwamuzi kwa madai kuwa alimsukuma kipa wa Yanga, Obren Cuckovic kabla ya kufunga.

Kocha Msaidizi wa Mtibwa, Mecky Maxime alisema vijana wake walicheza vizuri, lakini akamtupa lawama mwamuzi wa mchezo huo kuwa alikuwa akiibeba Yanga.

Kwa upande waYanga, Scolovisk alitimka baada ya mchezo huo bila kuzungumza lolote.

Katika mchezo wa jijini Dar es Salaam, Simba iliyokuwa imetawala mchezo, ilianza kuhesabu bao la kwanza katika dakika ya 17 lililowekwa kimiani na Hillary Echessa kwa mkwaju wa penalti baada ya Danny Mrwanda kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari.

Wachezaji wa pande zote walishambuliana kwa zamu kwa kukamiana, Julius Mrope wa Manyema ndiye aliyekuwa akiisumbua ngome ya Simba iliyokuwa chini ya Juma Nyosso na Kelvin Yondan.

Hata hivyo, timu zote zilipata pigo baada ya wachezaji wao, Haruna Moshi ‘Boban’ na Daudi Maganga kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Israel Nkongo baada ya kupigana uwanjani.

Pamoja na kucheza pungufu, Simba hawakutaka tamaa, walishambulia kwa nguvu na kupata la pili kwa penalti katika dakika ya 51 lililowekwa kimiani na Mrwanda baada ya Himid Mao kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la hatari.

Kocha wa Simba, Patrick Phiri aliwasifu wachezaji wake lakini akalalamikia kadi nyekundu kuwa mchezaji wake kuwa haikustahili. “Hapa mwamuzi amemuonea mchezaji wangu, hakustahili kwa kuwa kitendo kile ni rafu ya kawaida,” alisema Phiri.

Kocha wa Manyema, Abdallah Kibaden ‘King’ alisema wachezaji wake wamefungwa kutokana na kuzidiwa na swaumu. Hata hivyo, aliwasifu kuwa walijitahi kucheza vizuri.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments