FEDHA za mradi wa maendeleo ya soka za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) zimeiweka Kenya katika mzozo mwingine.

Mara hii, maofisa kadhaa waandamizi wa nchi hiyo wanadaiwa kuzitumia vibaya kwa maslahi yao binafsi.

Utata huo unamhusisha Katibu Mkuu wa kundi la Football Kenya Ltd, Sammy Obingo ambaye amesimaishwa dhidi ya ofisa mwingine kuhusiana na matumizi ya fedha hizo za mradi wa Goal Project.

Sehemu ya pili ya mradi huo ambayo inahusu ujenzi wa ofisi katika Kituo cha Kimataifa cha Michezo Moi, imekamilika, lakini maofisa waandamizi wa FKL wanamtuhumu Obingo kwa kuongeza gharama za ujenzi huo kiasi cha Shilingi milioni 7 za nchi hiyo (dola 100,000) bila ruksa.

Mwenyekiti wa FKL, Mohammed Hatimy aliliambia gazeti la The Standard kwamba ofisa huyo alisaini gharama za ziada za mradi huo na kuziwasilisha Fifa bila kibali cha bodi ya FKL.

“Gharama za mradi zilizoafikiwa ni ni Shilingi milioni 24 ( dola 342,000) na kiasi kingine cha Shilingi milioni 7 ( dola100,000) kilitakiwa kutumika kwa ukarabati.

Hata hivyo, kabla ya kukamilika kwa mradi, mkandarasi aliomba fedha zaidi na Fifa ikagoma kuzitoa,” alieleza mwenyekiti huyo.

“La kushangaza ni kuona kuwa Obingo alijipa mamlaka bila kibali na kuidhinisha gharama zaidi, kitu ambacho kimeiingiza nchi katika mgogoro mpya na Fifa , kitu ambacho ni sawa na ubadhirifu.

“Obingo hakuwa na mamlaka ya kusaini waraka huo, kwani mimi ndiye niliyesaini mkataba wa awali wa kandarasi hiyo. Yeye, alikuwa mwajiriwa tu. Tunashangaa ni kwa jinsi gani alivyojichukulia mamlaka, hiki ni nini zaidi ya ubadhirifu.”

Gazeti la The Standard limeeleza kuwa baada ya kuulizwa,Obingo alijitetea akisema kwamba alikuwa na mamlaka ya kusaini waraka huo wa matumizi ya ziada.

Alilionyesha gazeti hilo waraka mwingine wa mawasiliano na Ofisa wa Maendeleo wa Fifa, Ashford Mamelodi, akiomba mhandisi aandae waraka huo uliosainiwa na FKL na Fifa kabla ya malipo ya ziada kufanyika.

Mei 5, Mamelodi alieleza katika ujumbe wake wa email kwa mkandarasi huyo, “Tumeingia katika mgogoro wa kiufundi kuhusiana na malipo haya, tunataka tuelezwe sababu za kuomba malipo ya ziada.

“Tunapendekeza suala hilo limalizwe kwa njia hii, Fifa ilipe Shilingi milioni 5.6 (dola 80,000) mara moja, uandaliwe waraka wa ziada wa msanifu wa mradi ukionyesha mradi wenyewe, usainiwe na FKL, mhandisi na kisha usainiwe upya na Fifa.”

E-mail hiyo ya Mamelodi ilikuwa ikijibu maombi ya mkandarasi huyo aliyekuwa akiomba fedha kwa kazi ambazo alikuwa tayari amefanya.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments