Maximo kufanya mchujo leo

Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo.

Kocha mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo, amesema kuwa leo atatangaza majina ya wachezaji 20 ambao wataondoka nchini Jumanne kuelekea Rwanda kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na wenyeji wao, Amavubi.

Stars ambayo katika viwango vya ubora wa soka duniani iko katika nafasi ya 93 na Amavubi 117 wanatarajia kukutana kwenye uwanja wa Amahoro siku ya Jumatano.

Maximo alisema jana kuwa katika kikosi hicho atakachokitangaza hakitakuwa na beki wake mahiri, Shadrack Nsajigwa, Mussa Hassan ‘Mgosi’anayeshughulikia safari yake ya kwenda Norway na mshambuliaji, Jerryson Tegete ambaye bado hajapona vizuri maumivu ya mguu.

Alisema kuwa wachezaji wengine wote waliobakia wameweza kuonyesha uwezo mzuri katika mazoezi yake yaliyoanza Jumamatu iliyopita na hali hiyo imetokana na kila mmoja wao kufahamu jukume lake.

Maximo alisema kuwa juzi na jana alikuwa akiwafundisha zaidi jinsi ya kukaba na kufanya mashambulizi ya haraka ili waweze kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa kwanza wa kirafiki kwa timu yake kufanyika ugenini.

“Ni mechi muhimu sana kwetu, wachezaji wengi ni chipukizi na hii itakuwa ni mara ya kwanza kwao kucheza nje ya nchi, sina hakika sana na Tegete, ninataka kumuona Bocco (John) anavyokuwa kwa kuanza,” alisema kocha huyo.

Alisema pia leo timu yake itafanya mazoezi asubuhi na jioni huku timu ikifanya mazoezi mara moja ambapo watakuwa ufukweni.

Aliongeza kuwa hivi sasa katika mazoezi ya timu hiyo ushindani umezidi kuongezeka na hali hii anaamini inachangiwa na baadhi ya wachezaji kupata uzoefu katika klabu za nje, ambazo wamewahi kuzichezea na ushindani mwingine ulioko katika timu zao za hapa nyumbani.

Katika mchezo huo wa kirafiki, Stars inatarajia kuutumia kujiandaa na mashindano ya Chalenji yaliyopangwa kufanyika mwezi Novemba katika jiji la Nairobi, Kenya na mechi za kuwania kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (CHAN) ambazo zitaanza kuchezwa mapema mwakani.

Amavubi yenyewe inajiandaa na mchezo wake wa kufuzu kushiriki fainali za Kombe la Dunia dhidi ya timu ya taifa ya Misri, Pharaos ambao umepangwa kufanyika Septemba 5 katika jiji la Cairo. Hata hivyo katika mechi hiyo, Stars itawakosa nyota wake watatu ambao wako nje ya nchi hivi sasa, ambao ni Henry Joseph, Nizar Khalfan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

CHANZO: NIPASHE

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments