Tanzania yapaa kwa ubora wa Fifa

MECHI ya Tanzania na New Zealand miezi michache iliyopita imeendelea kuwa neema kwa Tanzania baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa, Fifa kuipandisha kwa nafasi nne zaidi mwezi huu.

Kulingana na viwango vya Fifa,Tanzania imepanda kwa nafasi nne kutoka 97 hadi 93, ingawa kwenye viwango vya CAF (Shirikisho la Soka Afrika) imebaki katika nafasi yake ya 23.

Kwa mujibu wa mtandao wa Fifa, Uganda ndiyo inayoongoza katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa kushika nafasi ya 75 na nafasi ya 15 katika bara la Afrika.

Tanzania ambayo wiki ijayo timu yake, Taifa Stars inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki na timu ya taifa ya Rwanda, Amavubi mjini Kigali, imezipiku Kenya iliyoko nafasi ya 105 kwa viwango vya Fifa na ya 28 kwa upande wa CAF.

Rwanda, ambayo kama Tanzania ni mwanachama wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), iko katika nafasi ya 117 katika ngazi ya Fifa na 31 barani Afrika. Burundi iko katika nafasi ya 128 na 35 katika Afrika.

Stars kwa sasa iko kambini jijini Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya Amavubi ya Rwanda itakayochezwa Agosti 12 mjini Kigali, mchezo ambao kocha Marcio Maximo amekuwa akiupa umuhimu mkubwa na kuonya kuwa endapo timu hiyo itashinda, ni wazi itakuwa imejitengenezea mazingira mazuri ya kupaa zaidi kwa ubora.

Tanzania iliichapa New Zealand ‘All Whites’ mabao 2-1 katika Uwanja wa Taifa miezi miwili iliyopita.

Mchezo huo ulikuwa mahsusi kwa New Zealand kujinoa kwa michuano ya Kombe la Mabara nchini Afrika Kusini ambako ilichapwa mechi mbili na kutoka sare moja.

Mchezo huo ambao ulihudhuriwa na mamia ya mashabiki na kuonyeshwa kwenye televisheni duniani kote kwa maombi ya wageni hao ambao waliahidi kuitangaza nchi na vivutio vyake kote duniani.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments