Timu ya Mzizima yatwaa umalkia kombe la Mzeru

Nahodha wa timu ya Mzizima Queen Sofia Mwasikili akikabidhiwa kombe na naibu waziri wa TAMISEMI Agrey Mwanri mara baada ya timu yake kutwaa ubingwa wa wanawake wa mashindano ya Mzeru Cup yaliyoandaliwa na Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini Dk Omari Mzeru, baada ya kuifunga Mchangani Queen mabao 5-0

TIMU ya Mzizima Queen imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Mzeru kwa wanawake baada kuichakaza Mchangani Queen kwa mabao 5-0 huku mshambuliaji wake Asha Rashid ‘Mwalala’ akifunga mabao manne.

Mbali na mabao hayo manne yaliyofungwa na Mwalala, Mzizima iliundwa na wachezaji wa timu ya Taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Star’ ilipata bao lake la tano lilifungwa na Esta Chabuluma ‘Lunyamila’

Katika mchezo wa wanaume chini ya miaka 17 ,timu ya Bom Bom ya Dar es Salaam ilitwaa ubingwa huo baada ya kuifunga Taifa mabao 2-1 katika mchezo wa fainali ulioshuhudiwa na naibu waziri wa TAMISEMI, Agrey Mwanri.

Mabao ya Bom Bom katika mchezo huo yalifungwa na mshambuliaji wake Dulla Hugo huku la Taifa likifungwa na Bakari Selemani na katika umri wa miaka 14 timu ya Villa Squad ndio iliyotwaa ubingwa huo.

Akifunga michuano hiyo, Naibu Waziri wa TAMISEMI, Agrey Mwanri alimpongeza mbunge wa jimbo la mjini, Dk Omar Mzeru kwa kuandaa michuano hiyo itakayosaidia kukuza vipaji .

Mwanri alisema wizara yake itaangalia uwezekano wa kusaidia michuano hiyo ya kila mwaka kwa kuwa itaendana na ile ya UMITASHUMTA na UMISETA ambayo inalenga kukuza vipaji vitakavyotumiwa na taifa katika siku za baadae.

Naye mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Dk Mzeru alisema anatarajia kuiboresha zaidi michuano hiyo inayofanyika kwa mara tatu huku akilenga zaidi katika kuboresha zawadi kwa washindi.

Mzizima iliwasili jana jijini Dar es Salaam na kupokelewa na viongozi wa vyama vya michezo pamoja na Katibu mkuu wa Chama Cha Mpira wa Miguu Wanawake Mkoa wa Dar es Salaam (DWFA) Stephania Kabumba.

Akizungumza na Mwananchi kocha wa timu hiyo Nowa Kanyaga alisema Mzizima imekuwa bigwa kutokana na maandalizi mazuri.

“Mandalizi tuliyoiyandaa timu yetu ndiyo yameipa ushindi” alisema.

Naye nahodha wa timu hiyo Sofia Mwakisiri alisema licha ya kushinda michezo yote, lakini kulikuwa na ushindani mkubwa.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments