TFF yapata mkataba mnono wa Sh5.85bilioni toka Marekani

Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela, taasisi yake imepata udhamini mnono.

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limepata udhamini wa dola zaidi ya 4,5000,000 (Shilingi bilioni 5.85za Tanzania ) kutoka Kampuni ya +One Fashion USA Corporation ya Marekani.

Mkataba huo wa miaka minane, pamoja na mambo mengine utaliwezesha shirikisho hilo kupata fedha taslimu, motisha nyingine nyingi kwa timu zake mbalimbali ambazo ni Taifa Stars , ile ya wanawake, Twiga Stars na vijana, chini ya miaka 23, 20 na 17.

Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema jana kuwa katika mkataba huo, kampuni hiyo itatoa fedha taslimu, dola za Marekani 50,000 kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne ya kwanza.

Aliongeza kuwa kampuni hiyo pia itagharamia michezo minne ya kimataifa ya kirafiki ambayo Stars itacheza ndani au nje ya nchi na kwamba wadhamini hao pia watalipia gharama zote za timu hiyo kusafiri nje.

Kulingana na mkataba huo, pia timu ngeni zitaweza kufika nchini ikiwa ni pamoja na wadhamini hao kuandaa mashindano maalum kila mwaka yatakayojumuisha timu za mataifa manne, ikiwemo Tanzania.

Aidha, kampuni hiyo itatoa dola 75,000 kwa mwaka kwa miaka minne ya awamu ya pili. Awamu zote zikiwa za fedha taslimu, dola 500,000.

Pia, fedha taslimu 20,000 zitatolewa kwa TFF kama zawadi kwa Stars endapo itafikia nusu fainali ya Kombe la Chalenji, ambalo mwaka huu litafanyika nchini Kenya.

Stars, pia itapewa dola 50,000 ikiwa itafuzu kwa fainali za Kombe la Dunia. Pengine zikianzia kwa fainali za mwaka 2014 nchini Brazil.

Kadhalika, katika mkataba huo, Stars itapewa dola 25,000 kama itafuzu kwa fainali zozote za Afrika. Fainali hizo ni zile za wachezaji wa ndani (CHAN), ambazo zitafanyika Sudan mwaka 2011 na (Mataifa ya Afrika), CAN mwaka 2012.

Kwa upande wa vijana, mkataba huo utawezesha timu hizo, chini ya miaka 17 na 20 kupata dola 25,000 taslimu kwa kufuzu kushiriki Kombe la Dunia, kama ilivyo kwa Twiga Stars.

Mwakalebela alisema mkataba huo ni wa miaka minane na umesainiwa rasmi Juni 20 mwaka huu na kwamba chini ya udhamini huo, TFF itanufaika kwa kupata vifaa bora vyenye kiwango cha kimataifa.

Alisema kila mwaka kampuni hiyo itatoa sare za kuchezea michezo 900, sare za mazoezi 900, soksi za michezo 1,200, soksi za mazoezi 1,200, suti za michezo 400.

Vifaa hivyo ni pamoja na suti za mazoezi wakati wa mvua 400, polo shirt 500, mavazi wakati wa mapumziko ambayo ni kaptula na suruali 500, mipira ya mazoezi 500, viatu vya michezo jozi 500, viatu vingine vya wanamichezo jozi 500, vikinga ugoko jozi 500, taulo kubwa 200, mabegi ya safari 500, kofia 250, sare za mlinda mlango 100, gloves za mlinda mlango 100 na taulo ndogo za wachezaji za kufutia nyuso 300.

Vifaa hivyo vyote vitakuwa na thamani ya dola za Marekani 450,000 ambayo ni sawa na dola 3,600,000 kwa miaka nane.

Alisema kampuni hiyo pia itajikita kwa maendeleo ya vijana ambayo itatoa sare 300 kwa ajili ya makundi ya vijana kila sare itajumuisha jezi, kaptula na soksi, mipira 300 kwa ajili ya programu za mafunzo ya vijana, Bibs kwa ajili ya mafunzo ya vijana wadogo, mafunzo kwa watoto kuanzia miaka 8 hadi 17 na msaada wa kiufundi iwapo TFF itahitaji.

“+One itatengeneza jezi za timu ya taifa pamoja na vitu vingine ambavyo vitauzwa kwa mashabiki na TFF kupata asilimia 10 ya mapato…TFF na wanachama wake wataweza kununua vifaa hivyo kwa punguzo la bei.

Alisema kabla ya kufikiwa kwa mkataba huo, TFF ilipitia mikataba ya makampuni kama Adidas, Nike na Global Scouting Bureau (GSB) ya Marekani na kubaini kuwa ule wa +One una manufaa zaidi kwa maendeleo ya mchezo wa soka.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments