Tanzania na netiboli

MKAGUZI wa maandalizi kwa ajili ya michuano ya kimataifa ya netiboli kutoka Shirikisho la Netibali la Kimataifa (IFNA) kwa Ukanda wa Afrika amethibitisha kufanyika kwa mashindano hayo nchini baada ya kuridhishwa na mazingira ya uwanja na malazi.

Joan Smit, kutoka nchini Afrika Kusini alisema jana kuwa ameridhishwa na Tanzania kuweza kuandaa mashindano hayo kutoka na kukidhi vigezo vya kimataifa.

Timu nane zimethibitisha kushiriki mashindano hayo ya kimataifa ambazo ni Swaziland, Botswana, Marekani, Malawi, Lesotho, Ireland, Namibia, Shelisheli na Tanzania. Michuano hiyo itaanza Septemba 28 hadi Oktoba 3 mwaka huu.

Ofisa huyo alikipongeza Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta) kwa kuandaa michuano hii mikubwa pamoja na Serikali ya Tanzania kukiruhusu chama hicho kufanya mashindano hayo ambayo ndiyo yanategemewa kuwa ya kwanza kufanyika barani Afrika.

”Lakini, ninawapongeza pia kwa wapenzi wa mchezo huo, Watanzania kwa ujumla kujitokeza kuchangia kwa hali yeyote kama pesa,usafiri au kushangilia michuano hii itakapokuwa ikifanyika.”

Tayari, Kampuni ya kuuza vifaa vya michezo, Gilbert ya Afrika Kusini imejitokeza kuuza vifaa vya michezo wakati wa michuano hiyo.

”Kampuni ya Gilbert iko maalum kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya vifaa vya michezo ili kusitokee upungufu wowote na hasa katika michuano hiyo mikubwa , lakini pia wafanyabiashara wengine wanaweza kununua vifaa kwa bei nafuu,” alieleza.

Mkaguzi huyo ambaye aliwasili nchini juzi na ataondoka leo. Alikuwa nchini kwa lengo la kukagua uwanja, vyumba vya kupumzikia wachezaji na waamuzi , sehemu zitakapofikia timu na hoteli ya Blue Pearl, Dar es Salaam ndiyo imepata jukumu la kufikia kwa timu hizo.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments