Epukeni fujo-Serikali

WAKATI mabingwa wa bara la Oceanic, timu ya New Zealand ikitarajiwa kuwasili nchini leo usiku,Serikali imewaonya mashabiki na wadau wa soka nchini kuepuka kufanya fujo na kuzomea ili kulinda heshima ya nchi.

Mabingwa hao watakuja nchini kwa mafungu ambapo, fungu la pili linatarajiwa kuwasili kesho asubuhi, tayari kwa mchezo wa kirafiki wa Kimataifa dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ mchezo utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo, Florence Turuka alisema wanatoa rai kwa Watanzania wote watakaojitokeza siku hiyo uwanjani wadumishe nidhamu, ili waweze kufikia azma yao ya kuvutia wageni.

Alisema kadri watakavyoweza kutoa huduma nzuri na ya kuridhisha kwa timu hiyo, itakuwa ni kielelezo kizuri cha kuwavutia watalii wengi kupitia Tanzania, wakati wa kwenda au kutoka Afrika Kusini katika mashindano ya Kombe la Dunia mwaka 2010.

”Kwetu sisi Watanzania, mchezo huo ni kipimo kizuri kwa timu yetu na pia katika kuweka nchi mazingira mazuri kwa namna nchi itakavyofaidika na kunufaika na kombe la Dunia, tunahitaji utulivu siku hiyo,” alisema Turuka.

Alisema New Zeland kwa sasa ipo katika nafasi ya 78, katika viwango vya ubora wa Kimataifa vinavyotolewa na Shirikisho la  Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), ambapo hiyo pia ni fursa nzuri kwa Stars kushinda mchezo huo, ili isogee juu zaidi kwani mchezo huo utaingizwa katika viwango hivyo.

Turuka alisema mbali na kudumisha nidhamu, pia alitoa wito kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi, ili kuishangilia timu yao na kupata burudani ambapo tiketi za mchezo huo zitaanza kuuzwa leo, katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

Wakati huohuo, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Florian Kaijage alisema timu hiyo itafikia kwenye hoteli ya Paradise City, ikiwa na kikosi kamili ambapo wachache watawasili kesho asubuhi.

Pia alijibu swali aliloulizwa kuhusu viingilio vya mchezo huo kuwa ni vya juu ambapo cha juu ni sh. 40,000 na cha chini 5,000, alisema viingilio hivyo vinapangwa kulingana na mchezo husika. 

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments