Bendera: Vodacom, TFF, klabu mjadili mapya Ligi Kuu

NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera amesema ili kupunguza malalamiko, wadhamini wa Ligi Kuu Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom, Shirikisho la Soka tanzania, TFF na klabu kukaa pamoja na kuangalia upungufu uliojitokeza msimu uliopita.

bendera

Bendera aliyasema hayo juzi usiku katika hafla ya kutoa zawadi kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom kwenye Ukumbi wa Mikutano wa DICC, Dar es Salaam.

Katika hafla hiyo, mbali na Yanga kulamba Sh37mil za ubingwa, pia imetoa mfungaji bora, Boniface Ambani na kocha bora Dusan Kondic.

Wengine waliozawadiwa ni Simba Sh14milioni kwa kushika nafasi ya pili na Mtibwa Sugar walioondoka na Sh9mil. Mchezaji bora wa Ligi Kuu ni Oscar Joshua wa Toto African ya Mwanza na kipa bora ni Hassan Kado wa Mtibwa Sugar.

Timu yenye nidhamu ni Mtibwa Sugar wakati Mwamuzi bora aliyetajwa ni Ibrahim Kidilo wa Tanga.

“Nawapongeza Vodacom kwa kazi nzuri pamoja na wadhamini wengine, lakini sasa ninachotaka kuwaambia, mkae pamoja na viongozi wa klabu za Ligi Kuu, TFF mjadili upungufu uliojitokeza katika udhamini wa msimu huu na kumaliza kabisa kama si kupunguza kwa msimu ujao,” alisema Bendera.

Hatua ya bendera imekuja ikiwa ni mara kadhaa klabu kulalamikia utoshelezi wa udhamini wa Vodacom katika ligi hiyo kuwa bado haujawa wa kutosha.

Pamoja na kuwepo kwa kasoro hizo, mara kadhaa, TFF kupitia kwa Rais wake, Leodegar Tenga imekuwa ikihimiza kuwa Vodacom wanasaidia sehemu ya gharama na klabu inawajibika kusaka wadhamini wao.

Hata hivyo, pamoja na kuelezwa kuwepo na kasoro za hapa na pale katika ligi hiyo iliyomalizika kwa Yanga kutwaa ubingwa, wahusika wamezitumia kwa kuziba mashimo hayo baada ya kutumia zaidi ya Sh500mil mbali na Sh400mil zilizokuwa zimetengwa kwa msimu huu.

Meneja Uhusiano wa Vodacom, Emilian Rwejuna alikaririwa akisema Vodacom ilitumia Sh900mil nje ya kiwango kilichotajwa lakini lengo zima ni kuboresha ligi.

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano, Mkuu wa Udhamini na Uhusiano, George Rwehumbiza alisema kuwa Vodacom itaendelea kudhamini Ligi Kuu kwa kuwa mpango wa kampuni hiyo ni kuhakikisha soka ya Tanzania inapiga hatua pamoja na michezo mingine.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments