DRC yaipa kipigo Taifa Stars

Moja ya matukio wakati wa pambano kati ya Taifa Stars na DR Kongo katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam Jumamosi ambapo wenyeji walichapwa 2-0.

MABINGWA wa Afrika wa michuano ya wachezaji wa ligi za ndani (CHAN), Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) wameilemea Taifa Stars na kuilaza mabao 2-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki.

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dakika ya tano, Kaluyituka Dioko aliiandikia DRC bao la kwanza baada ya mabeki wa Stars kujichanganya katika kuokoa mpira wa kona.

Nafasi kubwa na pekee ambayo Stars wataijutia ni ile ya dakika 42 za kipindi cha kwanza ambayo Mrisho Ngassa alishindwa kuunganisha krosi ya Jerry Tegete.

Katika kipindi cha kwanza, DRC walitawala dakika 15 za kwanza kupitia kwa washambuliaji wake Bongeli Lofo, Dioko na Bokanga Eric ambao waliisumbua ngome ya Stars.

Baada ya hapo Stars walijitahidi kushambulia kwa kushtukiza kupitia kwa Ngassa, Mwinyi Kazimoto wakisaidiwa na Nurdin Bakari, lakini wakakosa umakini na mbinu za kumtungua kipa mwenye mbwembwe, Muteba Kidiaba.

Baada ya kosa kosa hizo, kwa mara ya pili, Kaluyituka aliwaduwaza tena Watanzania kwa bao baada ya kuunasa mpira na kumchanganya Nadir Haroub Cannavaro na kipa wake, Juma Dihile ambaye alionyesha kuwa mzito na kuandika bao kwa mkwaju wa umbali mrefu.

Ukiachana na matokeo hayo, mashabiki wengi waliofurika uwanjani hapo walionekana wakimzomea kocha Marcio Maximo na kumtolea maneno ya kashfa.

Lakini, tukio la uongozi wa Chama cha Soka cha DR Congo kuizawadia TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), klabu za Simba na Yanga kupamba mchezo huo wa kirafiki ambao uliandaliwa mahsusi na wenyeji, TFF kuipa mazoezi timu inayojiandaa kuikabili New Zealand mwezi ujao.

Kwa kiasi kikubwa, mabingwa hao wa Afrika walicheza mpira wa kawaida ambao hautofautiani na ule wa Stars. Kasoro kubwa ilikuwa ni wenyeji kutokuonyesha juhudi hasa kipindi cha pili cha mchezo huo.

Vikosi katika mchezo huo:

Stars-Shaaban Dihile,Shadrack Nsajigwa,Juma Jabu, Salum Sued, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Henry Joseph, Mrisho Ngassa, Nurdin Bakari/Jabir Aziz , Jerry Tegete, Nizar Khalfan/Mussa Mgosi, Mwinyi Kazimoto/Kigi Makassi

DRC- Muteba Kidiaba, Nkulukuta Miala, Kasongo Ngandu,Kimuaki Joel/Mukinayi Shani, Bokese Gradys, Mihayo Kazembe, Kaluyituka Dioko, Bedi Mbenza, Loto Bongeli, Bokanga Eric/Mabele.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments