Pongezi kwa Salim Mbonde, Charles Hilary, Halima Mchuka, Izengo Kadago. …

MARA nyingi katika makala zangu katika kona hii, wasomaji wangu mtakuwa mmegundua kuwa makala zangu zimekuwa zikijielekeza kutoa shukrani au kutoa pongezi kwa waliofanya vizuri michezoni, hivyo kusaidia maendeleo ya wachezaji kupitia nafasi zao kama makocha, viongozi wa timu, ufadhili na maeneo mengine.

Mtangazaji maarufu wa mpira wa enzi hizo akiwa shereheni.
Mtangazaji maarufu wa mpira wa enzi hizo. Salim Mbonde akiwa shereheni.

Kwa kutambua umuhimu wa kila mmoja katika maendeleo ya soka au michezo kwa ujumla, leo nitawazungumzia watangazaji waliokuwa wakitangaza wakati huo ambao ufanisi wa kazi yao ulichangia kwa kiasi kikubwa msisimko wa soka. Ikumbukwe, wakati huo teknolojia ya televisheni haikuwa imeenea kwa wingi, hivyo shabiki wa mpira wa kule Kigoma, Mpanda Rukwa, Nyamanolo, Mwanza, au Muleba, Bukoba, alipata taarifa kwa kusikiliza matangazo ya mpira kupitia redio.

Kutokana na umahiri wao katika utangazaji, mtu aliyesikiliza mpira akiwa kona yoyote ya nchi, aliweza kupata burudani ya kutosha na kuridhika kwa kile kinachotangazwa katika viwanja mbalimbali.

Hivyo basi watangazaji mbalimbali walifanya kazi nzuri kama Salim Mbonde, Bujaga Izengo Kadago, Halima Mchuka na wengineo ambao sijawahi kuwataja, lakini nitawazungumzia zaidi wale waliokuwa jirani zaidi na wachezaji wa soka.

Ni wazi, ukaribu wao na wachezaji, walikuwa kama ndugu na kwamba, licha ya ukaribu wetu na wao, hawakubadili mwenendo wa kazi yao kwa kutusifia tu pasipo sababu, bali walikosoa au kusifia palipostahiki.

Mfano, Dominick Chilambo ambaye kwa sasa ni marehemu, Charles Hilary anayetangaza Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) na Ahmed Jongo, aliyestaafu, ambao kwa hakika, sauti zao na ufasaha wa kuripoti kilichokuwa kikiendelea dimbani, vilitosha kuwa burudani kwa wasikilizaji.

Mtangazaji maarufu wa matangazo ya moja kwa moja ya mpira.
Mtangazaji maarufu wa matangazo ya moja kwa moja ya mpira.

Na hicho ndicho ambacho kimenifanya niwakumbuke watangazaji hawa ambao kwa hakika walitoa mchango wao mkubwa katika maendeleo ya michezo, hususan soka katika enzi zetu.

Walipokuwa wakitangaza kwa mfano kwenye Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam ambao sasa unaitwa Uwanja wa Uhuru, wapenzi ambao hawakuwepo uwanjani, walijiona kama wako uwanjani wanashuhudia kinachoendelea.

Baadhi ya mashabiki waliofika uwanjani lakini wakashindwa kuingia kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo kukosa fedha, wengi wao walibaki nje na redio zao ndogo wakifuatilia matangazo ya mechi na kupata uhondo kama wako jukwaani katika uwanja huo.

Wengi wa watu hawa, ni wale waliokuwa wakifika uwanjani, lakini wakishindwa kuingia kwa kukosa fedha, hivyo kusubiri dakika za kuingia bure, ambazo kwa lugha ya kimichezo, huita ‘fungulia mbwa’, yaani wasio na fedha.

Cha kushangaza ni kwamba, baada ya filimbi ya mwisho, wale walioingia dakika chache kabla ya filimbi ya mwisho huku wakifuatilia dakika zaidi ya 80 kwa matangazo ya redioni, ukimuuliza kuhusu mechi hiyo, walikuwa wakitoa maelekezo mazuri kuliko hata yule aliyeshuhudia mechi husika kwa dakika zote 90.

Huu si umahiri tu wa shabiki, bali ni ufasaha pia wa mtangazaji wa mechi kwa jinsi alivyokuwa akiripoti matukio ya mechi hiyo hata kumfanya msikilizaji kujiona kama yuko kwenye jukwaa akishuhudia mechi.

Nakumbuka jinsi baba yangu, mzee Luwongo, katika uhai wake alivyokuwa akitayarisha redio yake kujiwekea mazingira mazuri ya kusikiliza redio, utadhani yupo uwanjani akifuatilia!

Wakati wapenzi na mashabiki wakifurahia kupata maelezo ya mechi kwa ufasaha mkubwa, nasi wachezaji tulio wengi, sifa zetu zilikuwa zikinogeshwa na watangazaji hawa ambao licha ya kutangaza soka kwa kuwa na majina ya wachezaji, wao karatasi ilikuwa kama kutimiza wajibu tu.

Licha ya kuwa na karatasi za majina ya wachezaji, lakini wengi wao hawakuwa wakitegemea karatasi, kwani kutokana na kuwa karibu na wachezaji, waliwajua wengi kiasi kwamba, hawakuwasumbua hata katika kutangaza.

Mtangazaji wa mpira mwanamama wa kwanza katika Tanzania, akiwa na akina mama wengine maarufu katika fani ya utangazaji
Mtangazaji wa mpira mwanamama wa kwanza katika Tanzania, akiwa na akina mama wengine maarufu katika fani ya utangazaji

Binafsi, niliwahi kushuhudia Charles Hilary akitangaza mechi ya Sigara na Red Star katika Uwanja wa Uhuru bila kuwa na karatasi. Tukiwa katika chumba cha utangazaji pale Uwanja wa Uhuru, aliweza kutangaza kwa ufasaha bila hata ya kukosea majina.

Aidha, ndivyo ilivyokuwa kwa Dominic Chilambo, ambaye kwa sasa ni marehemu, ambaye katika uhai wake, ndiye alikuwa mwasisi wa jina la TP Lindanda. Hili lilikuwa jina la utani la Pamba ya Mwanza wakati huo ikiwika kwelikweli katika soka ya Tanzania.

Ninapokumbuka umahiri wa Chilambo, naishia kusema, Mungu amuweke mahali pema peponi! Amina.

Huku majina ya Khalfani Ngassa, Raphael Paul, Ali Bushiri, Hussein Marsha, Abdalah Bori, Kitwana Suleiman, David Mwakalebela, Rajabu Risasi, Rashidi Abdalah, Ibrahim Magongo, George Masatu, Nico Bambaga, Beya Simba na wengineo wa Pamba, yakipambwa vilivyo na Chilambo.

Chilambo, alikuwa na uwezo wa kumpatia picha kamili ya mchezaji kiumbo, kiuchezaji, kitabia, kitu ambacho ni watangazaji wachache wamejaliwa katika kutimiza wajibu na kazi zao.

Usiulize kuhusu kaka yangu, Ahmed Jongo, ambaye alikuwa ndiye kaka wa wachezaji wa timu ya Maji Maji ya Songea waliopata umaarufu mkubwa wakati alipokuwa akitangaza kule Radio Tanzania-Ruvuma.

Beki mstaarabu, Samli Ayubu, Celestine ‘Sikinde’ Mbunga, Octavian Mrope, Dadi Athumani, Madaraka Suleimani, Ibrahim Mbuzi, Abdalah Waswa, Abdalah Chuma, Ahmed Kampira, Maulid Toffi, wote hawa walikuwa Maji Maji, ambao walipaishwa vilivyo na Jongo.

Hizi hazikuwa sifa za kusukwa tu, bali ilikuwa ni sifa halisi za wachezaji hao zilizokuwa zikielezwa na watangazaji hawa hata kuwapatia taswira halisi ya wachezaji bila kuwaona kwa macho.

Naye rafiki yetu Charles Hilary, licha ya kuwapa sifa wachezaji wengi wa nchi hii hususan wa Simba na Yanga, lakini chachu ya maendeleo ya timu iliyokuwa ngeni katika Ligi ya mwaka 1986 ya Tukuyu Stars hata kutwaa ubingwa, kwa kiasi kikubwa kulichangiwa na kupambwa na Hilary.

Nikiwa mmoja katika kikosi kile, Hilary alikuwa akitupamba kwa sifa tulizostahili licha ya ugeni wetu katika Ligi Daraja la Kwanza (Ligi Kuu), kwani kwetu ilitosha kututia moyo sisi wachezaji.

Tulichokuwa tukifanya wachezaji, ni kurekodi mchezo mzima kwenye ‘kaseti’ na baada ya mechi, tulikwenda kuusikiliza na kuwa burudani kwetu, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kujituma zaidi katika mechi zinazofuata.

Nakumbuka mechi yetu ya nne katika ligi hiyo ya 1986, Charles Hilary ndiye alikuwa mtangazaji dhidi ya Yanga, mechi ambayo ilipigwa Uwanja wa Uhuru, ambako alitusifia tangu tulipoingia uwanjani kuanzia maumbo yetu, hata kutia madoido kuwa, pengine hatukuwa Watanzania, bali kutoka Nigeria, kwani tulikuwa warefu na miili mikubwa tukipambwa na weusi tii.

Hiyo ilitosha kutujenga kisaikolojia kwani tulijiona maumbo yetu yanatosha kuwafunga Yanga, hivyo hakuna sababu ya kupoteza mechi ile, kweli tulifanikiwa kuwafunga mabao 2-1.

Baada ya mechi hiyo, Hilary alisikika akisema, kwa Tukuyu kuifunga Yanga, hakuna timu ambayo ingeifunga Tukuyu katika msimu ule wa 1986, kwa sababu tulikuwa na kila kitu.

Kwa kweli maneno yake hayo yalitupa hamasa kubwa mno muulize Godwin Aswile, Mbwana Makata, Karabi Mrisho, Kelvin Haule, Yusuph Kamba, Aston Pardon, Danford Ngessy, Peter Mwakibibi, John Alex, Daniel Chundu, Ally Kimwaga na wengine tuliokuwa Tukuyu Stars tulivyopambwa kutokana na kujituma kwetu uwanjani na Charles Hilary.

Siyo hao niliowataja katika makala hii, bali walikuwepo wengine wengi ambao utangazaji wa kina Chilambo, Hilary, Jongo na wengineo mahiri kwa wakati huo, ulichangia kuchochea ari kwa wachezaji na timu kwa ujumla.

Binafsi, nawaombea heri kwani mchango wao ulikuwa chachu ya mafanikio ya wachezaji wengi wa zamani waliotangulia mbele ya haki na wengineo ambao bado tunapumua.

Ndiyo maana ninasema kwa dhati kabisa, mimi ni miongoni mwa wachezaji wa zamani ambao nilinufaika kwa kiasi kikubwa kwa upande wa soka kutokana na hamasa ya watangazaji hawa. Mwenyezi Mungu awazidishie heri!

Mwandishi wa Makala hii ni mchezaji wa zamani wa soka aliyewahi kuwika na timu kadha wa kadha kama Tukuyu Stars, Simba, Yanga na Taifa Stars.

Mbali ya kucheza, pia amewahi kufundisha timu kadhaa kama Singida United, ambaye kwa sasa anamiliki kituo cha michezo cha Tanzania Sports Catalyst (TSC).

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments