Man utd, nyanya kwa Liverpool

NDOTO za Manchester United kuongoza kwa pointi 10 na kuzidi kulikaribia taji la ubingwa wa Ligi Kuu zimeingia doa baada ya kukubali kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Liverpool.

Wakitumia makali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ambayo Jumanne yaliinyoa Real Madrid kwa mabao 2-0 na kufuzu kwa robo fainali, Liverpool waliingia kwa kasi katika Uwanja wa Old Trafford, ingawa walikuwa Man United waliokuwa wa kwanza kuandika bao kwa mkwaju wa penalti wa Cristiano Ronaldo.

Kama vile ilikuwa ni siku nzuri kwao, Liverpool ambao walishinda pia mechi ya kwanza, uwanja wa nyumbani, Anfield kwa mabao 2-1 walirejesha mabao hayo kupitia kwa Fernando Torres na nahodha Steven Gerrard katika kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, vijana wa Rafa Benitez ambaye alipata ushindi wa kwanza Old Trafford kwa miaka mzaidi ya mitano waliendelea kutawala na kufanikiwa kupachika mabao mengine mawili kupitia kwao, Fabio Aurelio kwa mkwaju wa adhabu ndogo na beki Andrea Dossena aliyekamilisha siku mbaya kwa vijana wa Alex Ferguson.

Beki wa kati wa Man United, Nemanja Vidic ndiye aliyeizawadia Liverpool bao la tatu baada ya kumkwatua Gerrard na kupewa kadi nyekundu na mwamuzi, hivyo kumpa nafasi Aurelio kuachia mkwaju ambao ulimpita kipa Edwin van der Sar akiukodolea macho.

Ushindi huo wa kwanza kwa vijana wa Benitez umepunguza tofauti ya pointi baina yao na United na kubakia pointi tatu, ingawa United bado wana mechi moja mkononi.

Timu hizo zilianza mchezo kwa kubadili vikosi vilivyocheza mechi za Ulaya kwa Man United ikimchezesha Carlos Tevez badala ya Dimitar Berbatov,Anderson na Park Ji-Sung kuziba nafasi za Ryan Giggs na Paul Scholes. Watatu hao, hata hivyo waliingia kipindi cha pili

Nao Liverpool, walimchezesha Lucas Leiva badala ya Xabi Alonso ambaye ni majeruhi, mkongwe Sami Hypia akiitwa kuchukua nafasi ya Alvaro Arbeloa ambaye aliumia jana wakati akipasha mwili kujiandaa kwa mechi hiyo.

Vikosi:

Manchester United: Van der Sar, O’Shea, Ferdinand, Vidic, Evra, Ronaldo, Carrick (Scholes, 74), Anderson (Giggs, 74), Park (Berbatov, 74), Rooney, Tevez.

Liverpool: Reina, Carragher, Hypia, Skrtel, Aurelio, Mascherano, Lucas, Kuyt, Gerrard (El Zhar, 90), Riera (Dossena, 68), Torres (Babel, 81).

Comments