Wanariadha toka mkoa wa Arusha wang’ara mbio za nyika

WANARIADHA kutoka Mkoa wa Arusha wamefanya vizuri katika na kuongoza mbio za nyika wanaume, wavulana na wasichana, huku ubingwa wa mbio za nyika wanawake ukichukuliwa na mwanariadha kutoka Zanzibar.

Wakimbiaji wakikimbia katika mitaa ya dar
Wakimbiaji wakikimbia katika mitaa ya dar

Mbio hizo za nyika zilizofanyika katika viwanja vya Moshi klabu zilifana, isipokuwa mikoa mingi iliyothibitisha kushiriki michuano hiyo haikujitokeza.

Mashindano ya mbio za nyika yaligawanywa katika makundi manne ya wanaume kilometa 12,wanawake kilometa 8, wavulana kilometa 8 na wasichana kilometa6.

Katika mbio za km.12 wanaume ambapo kulikuwa na washiriki wapatao 74, Faustine Mussa kutoka Arusha aliibuka mshindi baada ya kukimbia kilomita hizo kwa kutumia dakika 37:47:75.

Nafasi ya pili ilichukuliwa na Shamba Gitini kutoka Manyara ambaye alitumia dakika 38:18:59, na nafasi ya tatu ilichukuliwa na mwanariadha kutoka Manyara aliyetumia dakika 38:26:53.

Kwenye mbio za wanawake km.8 ambazo washiriki walikuwa 24, Jacquiline Sakilu kutoka Zanzibar alishinda mbio hizo kwa kutumia dakika 30:12:52 na nafasi ya pili ilichukuliwa na Sarah Kavina kutoka Arusha aliyetumia dakika 30:17:18 na nafasi ya tatu alikuwa Zaituni Jumanne kutoka Manyara aliyetumia dakika 30:58:41.

Mwita Marwa wa Arusha alishinda mbio za wavulana km.8 zilizoshirikisha washiriki 45 kwa kutumia dakika 25:26:82, mshindi wa pili alikuwa ni Alphonce Felix wa Arusha aliyetumia dakika 25:45:08 na nafasi ya tatu ilichukuliwa na Sylvester Naali wa Arusha, pia aliyetumia dakika 25:53:23.

Kwa upande wa wasichana, Mary Naali kutoka Arusha alishinda mbio hizo kwa kutumia dakika 21:35:0, ambapo nafasi ya pili ilichukuliwa na Failuna Abdul kutoka Arusha aliyetumia dakika 24:59:0 na nafasi ya tatu alichukua Mwanaidi Juma kutoka Arusha ambaye alitumia dakika 22:19:38.

Akizungumza baada ya kutoa zawadi, Meya wa Manispaa ya Moshi, Lameck Kaaya ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo alisema wakati umefika ambapo michezo mashuleni inatakiwa iwe imerudi kivitendo na kuwe na walimu wa michezo wa kuajiriwa katika kila shule.

Alisema suala la kodi katika vifaa vya michezo ni tatizo pia, hivyo serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo inatakiwa kupigania kuondoa suala la kodi ili kuhakikisha vifaa vya michezo vinapatikana kwa urahisi na kwa wingi nchini.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha nchini (RT), Suleiman Nyambui alisema walitarajia zaidi ya wanariadha 300 wangeshiriki mashindano hayo kama kila mkoa kati ya mikoa 26 ungetoa wanariadha 24, lakini mikoa iliyoshiriki ni michache na idadi ya wanariadha haikufika zaidi ya 200.

Alisema mikoa iliyoleta wanariadha ni Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Mara. Zanzibar ambayo ilileta wanariadha waliotoa ushindani wa uhakika.

Nyambui alisema tatizo la mikoa mingi kushindwa kushiriki ni kukosa fedha za maandalizi mikoani na nauli ya kuhudhuria mashindano ya mbio za nyika kitaifa.

Aidha, mwakilishi wa Kampuni ya Kuhudumia Makontena Bandarini (TICTS) waliodhamini mashindano hayo, Jay New alisema wataendelea kudhamini mashindano ya kitaifa ya riadha yanayoandaliwa na shirikisho hilo la riadha nchini.

Mshindi katika mbio hizo za nyika katika kila kundi alipata Sh80,000, mshindi wa pili, Sh 70,000, wa tatu Sh60,000, mshindi wa nne Sh50,000,mshindi wa tano, Sh40,000, mshindi wa sita Sh30,000, mshindi wa saba Sh20,000 na mshindi wa nane Sh10,000.

Mbio za nyika kimataifa zinatarajiwa kufanyika Jordan mwishoni mwa mwezi huu, wanariadha walioshinda mbio za nyika mkoani Kilimanjaro wanatarajia kushiriki katika mashindano hayo.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments