TFF yatakiwa imzuie Maximo

Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, limeombwa kumbembeleza Kocha Mkuu wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, Marcio Maximo, asiondoke mara mkataba wake utakapomaliza hapo Julai, ili aweze kuendeleza aliyoyaanzisha.

Hatahivyo, imeelezwa iwapo kocha huyo Mbrazil atakubali kuongeza mkataba basi apewe washauri wa ufundi kama Abdallah Kibadeni na Mohammed Msomali kumsaidia kufanya mambo kwa umakini tofauti na sasa.

benchi-la-taifa-stars
Mwenyekiti na Wachezaji wa soka wa zamani nchini, Khalid Abeid alipokuwa akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum, ambapo alisema kwa jinsi kocha huyo alivyoleta mabadiliko katika soka la Tanzania ni vema TFF imng’ang’anie asiondoke.

Abeid alisema kuwa TFF imbembeleze kocha huyo alegeze msimamo wake na kuongeza mkataba mwingine ili kutekeleza mipango yake ya miaka mitano aliyokuwa amejiwekea awali ambayo huenda ikainufaisha Tanzania kisoka.

“Kwa mafanikio aliyoyaleta Maximo ni vema kama angebakishwa ili kukamilisha mipango yake, lakini abadilishiwe mshauri wa ufundi ikiwezekana watu kama Kibadeni na Msomali ndio wapewe nafasi na tutanufaika,“ alisema.

Aliongeza kuwa kumuacha kocha huyo kuondoka itafanya Tanzania kurudi nyuma pale akija kocha mwingine mpya.

Kuhusu michuano ya CHAN itakayofanyika nchini Ivory Coast, alisema ana matumaini makubwa Tanzania kufanya vizuri ila aliwataka wachezaji kujituma na kuhakikisha wanashinda mechi yao ya kwanza kujiwekea mazingira mazuri.

“Kitu cha muhimu kushinda mechi yao ya kwanza na pia wachezaji wajitume na kutumia michuano hiyo kujitafutia soko la kimataifa, wasiende Ivory Coast wakiwa na hofu na naamini watafanya vema,“ Abeid kiungo nyota wa zamani wa Simba na Taifa Stars alisema.

Stars imefuzu kwenye michuano hiyo na imepangwa kundi A pamoja na timu mwenyeji Ivory Coast, Senegal na Zambia na itashiriki michuano hiyo miezi michache kabla ya Kocha Maximo kumaliza mkataba wake hapo mwizi Julai.

Mbrazil huyo alishawahi kunukuliwa kuwa mkataba wake huo wa mwaka mmoja utakapoisha ataondoka zake na inahusishwa kwenda Afrika Kusini.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments