Taifa Stars yapata unafuu michuano CHAN

ZAMBIA ikijiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani(CHAN), imekimbiwa na wachezaji watano tegemeo, huku Mike Baraza wa Kenya akisisitiza kwamba Taifa Stars itafanya maajabu Ivory Coast.

Katika michuano hiyo inayoanza Februari 22, Stars imepangwa kundi A na wenyeji Ivory Coast, Senegal na Zambia ambayo kocha wake, Mfaransa Herve Renald amechanganyikiwa baada kwa nyota wake aliowatengeneza kwenye kombe la chalenji Jijini Uganda, kukimbilia Ulaya.

stars-4

Mshambuliaji Rodger Kola wa Zanaco ndio wa mwisho kuondoka juzi kuelekea Sweden huku wachezaji tegemeo, kwenye ulinzi, Emmanuel Mbola, Francis Kasonde, kiungo William Njobvu na mshambuliaji matata Given Singuluma wakiwa wameshatua Ulaya.

Renard alisema; “Siogopi lakini inasumbua kupoteza wachezaji watano tegemeo mwezi mmoja kabla ya CHAN. Ni vigumu kufanya kazi na wachezaji wapya ukiwa na muda mfupi.”

Huku wachezaji hao ambao ni roho ya Zambia wakipepea na Tanzania ikichekelea, Baraza amesema kwamba anaamini uwezo wa wachezaji wa Tanzania hivyo hana wasiwasi na utendaji wa kikosi hicho.

“Tanzania nimeona ina wachezaji wengi sana wazuri na kikosi chake nilichokiona kule kwenye Chalenji Uganda ni kizuri nakiamini,”alisema Baraza.

“Naamini kwamba ikienda kwenye mashindano ya CHAN mwezi ujao itafanya vizuri, wachezaji wake wanaweza kushindana hata kwenye ligi za ndani wanafanya vizuri sana ni matokeo mazuri.

“Nawapa nafasi kubwa kwenye kundi lao,”aliongeza mchezaji huyo huku akisisitiza kuwa hana mpango wa kuondoka Yanga hadi atimize malengo yake.

Baraza ambae ni mkongwe alisema kwamba endapo juhudi zitaongezwa Tanzania itaiwakilisha vizuri kanda ya Afrika Mashariki na Kati(CECAFA) kwenye CHAN.

Stars ambayo ndio pekee iliyofuzu kwa ukanda wake, imeanza kuhofiwa na wenyeji ambao kocha wao Kouadio George amewanyooshea vidole Mrisho Ngassa, Henry Joseph na Juma Jabu.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments