Simba yatinga nusu fainali

Simba imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya michuano ya soka ya Tusker baada ya kuilaza Prisons ya Mbeya 2-0 katika mchezo we kundi B uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameifanya Prisons kuaga mashindano hayo kutokana na kupoteza mechi yake ya kwanza ilipofungwa na Tusker ya Kenya 2-0, Jumanne iliyopita.

sports2
Tusker nayo imeungana na Simba kwenye nusu fainali, ambapo keshokutwa zitagombea nafasi ya kwanza.

Timu hizo zitakuwa zinagombea nafasi ya kwanza kutokana na kulingana baada ya kila moja kuwa na mabao mawili na pointi tatu.

Simba inayonolewa na Twalib Hilal ilistahili kuondoka na ushindi huo kutokana na kutawala sehemu kubwa ya mchezo.

Prisons, hata hivyo, ndio iliwashtua Simba kutokana na Ali Yussuf wa Prisons kukosa bao katika dakika ya kwanza baada ya kupiga shuti la pembeni na kutoka nje.

Simba nayo ilijibu shambulizi hilo katika dakika ya pili baada ya kipa Nelson Kimathi wa Prisons kupangua shutu kali lililopigwa na Ulimboka Mwakingwe.

Baada ya muda mrefu wa kuisakama Prisons, Simba iliweza kupata bao la kuongoza katika dakika ya 27 lililofungwa na Ramdhan Chombo `Redondo` baada ya kupiga mpira wa faulo uliotinga moja kwa moja wavuni.

Bao hilo lilizidi kuichochea Simba na kuweza kujipatia bao la pili lililozamishwa wavuni na Mussa Hassan `Mgosi` katika dakika ya 37, ambaye alimalizia kazi nzuri ya Emeh Izechukwu.

Prisons ilipoteza nafasi nzuri ya bao baada ya Oswald Morris kupiga shuti lililotoka nje katika dakika hya 63 wakati kipa wa Simba, Amani Simba akiwa ametoka golini.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Simba, Hilal alisema alifurahishwa na ushindi huo kutokana na kuweza kurudisha imani ya wapenzi wake.

Hilal, hata hivyo, alionya kama kocha hakuwa ameridhishwa na kiwango cha uchezaji cha timu yake.

Kocha wa Prisons, James Nestroy alikubali kuwa timu yake ilizidiwa lakini alidai haikucheza vizuri kutokana na kuwa na wachezaji wengi wapya.

Timu zilikuwa:
Simba: Amani Simba: Salum Kanoni,. Juma Jabu, Meshack Abel, Kelvin Yondani, Henry Joseph, Ulimboka Mwakingwe, Mohamed Banka (Nico Nyagawa dk.66), Mussa Hassan `Mgosi`, Emeh Izechukwu na Ramadhan Chombo `Redondo'(Haruna Moshi `Boban` dk.77)

Prisons, Nelson Kimathi, Lusajo Mwakifamba, Laurin Mpalile, Sylvester Kamtande, Mbega Daffa, Lugano Mwangama, Henry Mwalugala (John Nditi dk.56), Hashim Selemani, Oswald Morris, Ally Yussuf na Ramadhan Katamba (Shabaan Mtupa dk.65)

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments