Stars we acha tu

Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, jana iliweka rekodi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani, baada ya kuifunga Sudan bao 2-1 katika mchezo uliofanyika Khartoum nchini humo, kwenye uwanja wa Al Hilal.

Tanzania kwa mara ya mwisho ilifuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 1980 ikiwa ni takribani miaka 28 iliyopita.


Stars, imefuzu kwa fainali hizo za Mataifa ya Afrika zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani, baada ya kuifungisha virago Sudan kwa jumla ya mabao 5-2 kufuatia ushindi wa 3-1 wa Stars iliyoupata katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika, ambapo kwa mara ya kwanza ilishiriki mwaka 1980 fainali hizo zilipochezwa Nigeria.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera ambaye jana alikuwepo uwanjani kushuhudia, mwaka 1980 alikuwa kocha wa Stars iliyoshiriki fainali hizo za Afrika.

Stars iliandika bao la kuongoza katika dakika ya tisa lililowekwa kimiani na Henry Joseph baada ya kazikubwa kufanywa na Mrisho Ngasa aliyeinyanyasa ngome ya Wasudan na kutoa pande kwa mfungaji aliyeukwamisha wavuni.

Hatahivyo, mchezo wa kujihami wa Stars, ulisababisha Sudan kupata bao la kusawazisha katika dakika ya 45 na hivyo kuwaweka roho juu wa Tanzania waliokuwa wakisubiri kwa hamu ushindi wa timu yao.

Timu ya taifa ya Tanzania ilipata bao la pili katikati ya kipindi cha pili lililofungwa na Nurdin Bakari, na kuihakikishia timu hiyo nafasi ya kwenda Ivory Coast mwakani kushiriki fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za nyumbani tu.

Stars katika mbio zake za kusaka nafasi ya kwenda Ivory Coast ilifungwa 1-0 na Kenya huko Nairobi Machi 29 kabla ya kuifunga Harambee Stars kwa bao 2-0 Aprili 12 jijini Dar es Salaam, na kuibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Uganda katika mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Mei 3 na kutoka sare ya 1-1 katika mchezo wa marudiano uliofanyika Kampala Mei 17 mwaka huu.

Ofisa Habari wa TFF, Shirikisho la Soka Tanzania, Florian Kaijage alisema kwa njia ya simu kuwa kocha wa Stars, Mbrazil Marcio Maximo alisema kuwa mchezo ulikuwa mgumu kama alivyotarajia, lakini anachoshukuru ni kwa wachezaji wake kufuata maelekezo na kupata bao la mapema lililowachanganya Sudan.

“Nilijua Sudan wakiwa kwao watashambulia sana na mchezo utakuwa mgumu, lakini niliwaambia vijana wangu na ninachoshukuru walifuata maelekezo na kupata bao la mapema lililowachanganya Sudan, tunashukuru tumefuzu kwenda Ivory Coast, “Kaijage alimkariri Maximo aliyezungumza baada ya mchezo huo.

Timu inatarajia kurejea nchini kesho saa 3 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways.

Kikosi cha Stars kilichoanza:Juma Dihile, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Salum Swed, Nadir Haroub Canavaro, Geofrey Bony, Mrisho Ngasa, Henry Joseph, Haruna Moshi, Jerson Tegete na Nurdin Bakari.

  • SOURCE: Lete Raha

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments