Tenga, Malinzi wamwaga sera

Leodegar Tenga na Jamal Malinzi juzi usiku walikutana uso kwa uso na kumwaga sera zao wakati wa mdahalo wa wagombea wa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la soka nchini (TFF) uliorushwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV.

Tenga na Malinzi watachuana kwenye kuwania nafasi ya Urais ya shirikisho wakati wa uchaguzi huo utakaofanyika Jumapili.


Wagombea hao walijinadi wakati wa kujieleza na kujibu maswali yaliyokuwa yanaulizwa na viongozi wa Chama cha Waandishi wa habari (TASWA) na wahariri wa michezo wa vyombo mbalinmbali vya habari wakati wa mdahalo huo ulioanza saa tatu na robo usiku.

Tenga, ambaye anatetea kiti cha urais, akionyesha kutulia, alikuwa wa kwanza kujieleza kwa kuelezea mafanikio ya miaka minne ya uongozi wake.

Alisema moja ya mafanikio yake imekuwa kubadili katiba ya TFF na kuhakikisha inasaidia uendeshaji wa shughuli za soka na pia ushirikiano aliopata kutoka kwa serikali na udhamini wa makampuni mbalimbali.

Tenga, alikiri bado kulikuwa na mapungufu katika katiba ya TFF na kuongelea kwa undani alipoulizwa juu ya migongano iliyokuwepo miongoni mwa kamati ndogo za shirikisho hilo.

Alikiri kulikuwa kuna matatizo ya katiba na hasa katika masuala ya rufaa na kufafanua pale Kamati ya Nidhamu chini ya Said El-Maamry ilipotengua maamuzi ya kamati ya utendaji kuiadhibu Yanga kususa kucheza na Simba kwenye mechi ya Kombe la Kagame.

Malinzi aliyeibuka katika mdahalo huo akiwa amevalia jezi ya timu ya taifa, Taifa Stars, alisisitiza lengo lake kubwa lilikuwa kuhakikisha soka mikoani inaendelezwa.

Alieleza akipewa ridhaa basi atavimbelea vyama vya mikoa na kuhakikisha vinakuwa na ofisi na vitendea kazi.

Ajenda nyingine ya Malinzi ilikuwa kuhakikisha TFF inakuwa na vitega uchumi na kutoa mfano wa uuzaji wa fulana za timu ya taifa.

Alipoulizwa amebuni vyanzo vipi vya mapato kutekeleza mpango huo mkubwa, alieleza akipata uongozi atabuni miradi ya kibiashara na kugeuza rasilmali za TFF kuweza kuwa vitega uchumi.

Ushindani mwingine ulikuwa kati ya wagombea Makamu wa kwanza wa Rais, ambayo inagombewa na Katibu Mkuu wa DRFA, Athumani Nyamlani, Katibu Mkuu wa zamani wa kilichokuwa Chama cha soka nchini (FAT), Ali Hassan Mwanakatwe na beki wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa Lawrence Mwalusako.

Nyamlani alitoa historia yake ndefu ya kupata kuongoza Chama cha soka cha Temeke (TEFA), DRFA na wakati fulani kuwa Afisa Tawala wa FAT.

Mwanakatwe alijinadi zaidi kwa kuwahi kuiongoza FAT na hivi sasa kufanya shughuli mbalimbali za Shirikisho la soka la Afrika (CAF) na lile la kimataifa (FIFA) na kujivunia programu za kuendeleza yosso katika shule ya Makongo na Jitegemee kiasi cha kumtaja kipa wa Yanga, Juma Kaseja.

Mwalusako alieleza kwa kirefu historia yake kama mchezaji wa zamani wa Yanga, Pan na timu ya taifa na elimu yake ya uchumi kiasi cha kuwahi kufanya kazi Benki Kuu ya Tanzania.

Pamoja na mchujo wao kufanyika, wagombea wa nafasi ya Makamu wa Pili wa Rais nao `walipigwa` maswali, ambao walikuwa ni Katibu Mkuu wa Yanga, Lucas Kisasa, Geoffrey Nyange, ambao walikwama na mwanasheria Damas Ndumbaro na Ramadhan Nasib waliopenya katika mchujo wa klabu uliofanywa jana.

Mdalaho ulioandaliwa na TASWA uliongozwa na mtangazaji wa Redio One, Deo Rweyunga, ambapo wahariri waliokuwa wakiuliza maswali walikuwa ni pamoja na Mwenyekiti wa TASWA, Boniface Wambura, Makamu wake, Tom Chilala na wahariri Frank Sanga (Mwanaspoti), Chaby Barasa (Daily News), Grace Hoka (Bingwa), Maulid Kitenge (Redio One) na Samson Mfalila (Nipashe).

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments