Kombe la Tusker: Yanga Uganda, Simba Kenya

MICHUANO ya Kombe la Tusker itaanza kutimua vumbi Desemba 15, lakini mabingwa watetezi Yanga wataingia uwanjani kuonyeshana kazi na URA ya Uganda siku mbili baadaye na watani zao Simba wakisubiri siku moja zaidi kucheza na Prisons ya Mbeya.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Yanga imepangwa Kundi A pamoja na URA na Mtibwa huku Simba ikiwa Kundi B na wababe wao Tusker FC ya Kenya na Prisons.

Katika mashindano hayo bingwa atajinyakulia Shilingi mil.40, na katika siku ya ufunguzi kutakuwa na mechi ya moja itayozikutanisha Mtibwa na URA huku Tusker na Prisons zikicheza siku inayofuata.

Yanga imeingia kwenye michuano hiyo kwa kujiamini kuwa wanaweza kutetea ubingwa wake kutokana na kusheheni kikosi imara ambacho kina wachezaji wengi wa kimataifa na pia wanaongoza Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa pointi 30.

Simba nayo ikiwa na historia ya kutwaa kombe hilo mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote imepania kurirudisha taji hilo mkononi mwake msimu huu baada ya mwaka jana kujitoa kwa madai wadhamini walitoa fedha kiduchu.

” Tuliwaachia tu Yanga, wenyewe tumerudi sasa baada ya wadhamini kuongeza fedha tunarejea kwa kasi na kulirudisha kombe letu,” alisema Mwina Kaduguda wakati akipokea vifaa jana kutoka kwa wadhamini wa michuano hiyo bia ya Tusker.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Fredirick Mwakalebela alisema Yanga na Simba imebidi zisubiri hadi Desemba 17 na 18 kutokana na wachezaji wake wengi kuwa timu ya Taifa Stars ambayo inaondoka wiki ijayo kucheza mchezo wa marudiano dhidi ya Sudan.

“Tutajitahidi kuhakikisha mashindano haya yanafanyika kwa mafanikio na yawe mashindano bora ya mfano wa kuigwa na kuiletea sifa nchi, wadhamini na yawe changamoto kwa timu ambazo hazishiriki.

“Ratiba hii imeangalia mambo mengi ikiwemo Simba na Yanga ambazo zina wachezaji wengi timu ya taifa na ndio maana mechi zao zinachezwa siku mbili baada ya kuanza kwa mashindano kwani nina uhakika Stars itakuwa imerejea kutoka Sudan na wachezaji watakuwa wamepumzika kwa siku mbili na kurudi katika klabu zao na kuendelea na mashindano ya Tusker,” alisema Mwakalebela.

Mwakalebela aliongeza kuwa mashindano hayo pia hayataathiri kambi ya Taifa Stars inayojiandaa kwa ajili ya michuano ya Challenge itakayoanza Desemba 31, Uganda.

” Kambi itaanza Desemba 27, lakini mazoezi rasmi yataanza Desemba 28 hivyo wachezaji wakimaliza fainali ambao wataitwa watajiunga na kambi hiyo kama kawaida hakutakuwa na athari zozote.”

Alisema Desemba 19 itakuwa ni mapumziko na Desemba 20 Yanga itacheza na Mtibwa Sugar na siku inayofuata Simba itaonyeshana kazi na Tusker ya Kenya.

Desemba 23 na 24 itakuwa ni nusu fainali na Desemba 26 na 27 zitakuwa ni mechi za kutafuta mshindi wa tatu na fainali.

Wakati huo huo Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Tusker imekabidhi vifaa vyenye thamani ya Sh milioni 80 kwa timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo.

Akikabidhi vifaa hivyo Meneja wa Bia ya Tusker, Sarah Munema alisema wamekabidhi vifaa hivyo ili kuhakikisha mashindano hayo yanakuwa ya kiwango cha juu.

” Bia ya Tusker inapenda kuendeleza ushirikiano kwa timu zinazoshiriki mashindano haya, vifaa hivi vitaiwezesha kila timu kushiriki kikamilifu ili ziweze kuelekeza nguvu na akili zao kwenye kushinda kombe.”

Timu zilizokabidhiwa vifaa jana ni Simba,Yanga, Tanzania Prisons pamoja na Mtibwa Sugar.

Bingwa wa michuano hiyo ataondoka na kitita cha Sh milioni 40, mshindi wa pili Sh milioni 20 na wa tatu Sh milioni 10.

Bingwa mtetezi wa kombe hilo ni Yanga huku Simba ikichukua mara nne tangu lianzishwe na mwaka jana timu hiyo ya mtaa wa Msimbazi haikushiriki kwa madai fedha kiduchu.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments