Wambura, Malinzi watemwa TFF

Aiyeuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF), Michael Wambura na Katibu Mkuu wa zamani wa Yanga, Jamal Malinzi wanadaiwa kutemwa katika kinyang`anyiro cha kuwania uongozi wa shirikisho hilo utakaofanyika Desemba 14.

Wambura anawania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Malinzi anagombea wadhifa wa Urais, ambao pia unawaniwa na Rais wa sasa, Leodegar Tenga.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana jijini zinasema kuwa Wambura ameondolewa na kamati ya usaili kufuatia majibu aliyotoa wakati wa usaili yanayohusiana na pingamizi alizowekewa kutoridhisha na hivyo kamati kuamua kumuengua.

Habari zaidi kutoka katika kamati hiyo zinasema kuwa Malinzi anadaiwa kuondolewa katika harakati hizo za kuwa `boss` wa TFF kutokana na vielelezo vilivyotoka katika klabu yake ya Yanga kushindwa kumthibitisha kuwa ameiongoza klabu hiyo katika muda alioutaja wakati anahojiwa.

“Subirini kamati itawatangazia lakini mambo yako mengi, sasa kama Malinzi ameshindwa kuwa na uthibitisho wa muda aliokuwa kiongozi Yanga, na pia hata ukianzia pale alipochaguliwa kuwa katibu mkuu hakuweza kumaliza muda wake kutokana na kujiuzulu,“ kilisema chanzo hicho.

Chanzo kingine kilisema kuwa Wambura na Malinzi wameondolewa kutokana na kutotakiwa kuwa viongozi katika shirikisho hilo kwa hofu kuwa wanaweza kuja `kuvuruga` misingi bora ya uongozi iliyowekwa na viongozi waliopo madarakani.

Akizungumza na Nipashe jana, Wambura alisema kuwa hata yeye habari hizo amezisikia tangu juzi baada ya kutoka katika chumba cha usaili.

Alisema kuwa taarifa hizo ni moja ya maneno yanayozungumzwa na watu mbalimbali ambao yeye hana uwezo wa kuwazuia.

Alisema kuwa anachosubiri ni kupata taarifa rasmi kutoka katika Kamati ya uchaguzi na baada ya taarifa hizo kama habari hizo zitakuwa zimetimia atatoa msimamo wake.

“Ni kweli hata mimi nimezisikia habari hizo, tena sio jana, tangu huko nyuma zilikuwa zinazungumzwa, kama itakuwa kweli itakuwa yametimia,“ alisema Wambura.

Mwenyekiti wa Kamati ya usaili, Henry Tandau alisema jana kuwa bado kamati yake inaendelea kufanyia kazi taarifa ambazo ilizipata baada ya usaili na baada ya kukamilika kwa zoezi hilo wataweka hadharani taarifa zote muhimu.

Tandau alishindwa kuweka wazi muda wa kutangaza taarifa hizo, lakini Makamu wake, Alex Mgongolwa alisema kuwa mambo yote yatatangazwa leo.

Alisema kuwa taarifa za leo pia zitahusiana na zoezi la usaili lililokuwa linawahusisha wadau waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa Chama cha Soka cha Wanawake Tanzania (TWFA) ambacho kinatarajia kufanya uchaguzi wake kesho.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments