Nataka kutengeneza wafungaji

LAURANCE MWALUSAKO

KATI ya wagombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Laurance Mwalusakon ‘Mwalu’ alirudisha fomu zake kwa staili ya aina yake.

Alitinga ofisi za Shirikisho la soka Tanzania, TFF saa 5:38 mchana akiwa na kundi la wachezaji wa zamani. Mwalusako anawania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais katika TFF.

Baadhi ya wachezaji hao ni wale waliowahi kucheza naye, waliomtangulia na ambao si wa muda mrefu, lakini wameshaachana na soka. Mwalusako alikuwa mchezaji wa Yanga.

Baada ya kuwasili TFF, akiwa mwenye bashabasha na kujiamini, alisema kuwa amechukua fomu kuwania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais akiamini kuwa anaweza kuitumikia nafasi hiyo.

Mwalusako ambaye ni msomi aliyetamba katika klabu ya Yanga na Taifa Stars anasema kuwa kilichomsukuma TFF ni kuona kuwa, kwanza watu wa mpira ndiyo wanaostahiki kuwemo TFF na suala la Taifa Stars.

Anasema: Hata ukiangalia katika vyama na mashirikisho mbalimbali ya soka, wanasoka wa zamani ndiyo wanaoongoza mpira, hakuna mtu ambaye si mwanasoka anayepewa nafasi sana.

“Hata hao walioingia hivi karibuni katika chama cha soka Poland katika mgogoro ulioingiliwa na FIFA, Rais aliyechaguliwa alikuwa mfungaji bora wa timu ya Poland Kombe la Dunia 1974.

“Sasa na sisi wachezaji wa zamani, ambao tunadhani tuna kila aina ya uwezo wa kuongoza, tuna kila aina ya utaalam, ndiyo tunatakiwa. Tunamuona mtu kama Mtemi Ramadhanui, yuko katika Utawala, TFF, Tenga Rais wa TFF, huku ndiko tunakotaka kufika.”

La pili ninalotaka kulisema ni hili la Taifa Stars. Timu yetu pamoja na kuimarika sana, lakini tatizo liko katika ufungaji. ”Mimi nasema ufungaji bado ni tatizo.

”Nilikuwa na mawazo ya kuwatengeneza vijana, kama nikiingia TFF, pamoja na mambo mengine, lakini nitakalosimama nalo ni kufanya mashindano, na wachezaji watakaoibuka wafungaji bora tuwapike.”

”Nimeona mashndano ya Copa Coca Cola, yamefanyika mara mbili, kuna wachezaji wanne, walioibuka kuwa wafungaji bora, sasa wale ndiyo wanatakiwa kutengenezwa, wapikwe kwa kila aina ya misaada naamini watatuletea mafanikio.

”Tatizo la ufungaji naamini litamalizika. Wafungaji wanatengenezwa, mchezaji akilala, akiamka anawaza mpira na kulenga shabaha, tunataka kuwa na wachezaji kama Didier Drogba, wawepo kama Samuel Eto’o, wawepo kama Thierry Henry….

”Inatakiwa kuwa na fowadi ya kutisha, kwamba timu mnacheza nayo inawaza itamkaba vipi fulani, inawaza itamkabili vipi mchezaji wenu, ndiyo maana timu inachezesha mtu hata kama mgonjwa ali mradi kuwachanganya wapinzani,” anasema.

Akizungumzia ya TFF, anasema kuwa wamefanya makubwa mengi na wanastahiki pongezi.

”kweli TFF wamefanya makubwa mengi, lakini bado kuna maeneo hayajaimarika. Vyama vya soka vya mikoa havijaamshwa, mikoani hakujakuwa na mwamko sana zaidi ya Dar es salaam.

“Soka inachezwa Dar es Salaam pekee, sasa nikiingia TFF, pamoja na kuwatengeneza vijana, kwa kushirikiana na wenzangu, naamini soka itachezwa katika kila mkoa pamoja na hamasa,” anasema Mwalusako.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments