Azamfc `yaizidi ujanja` TFF

Klabu ya soka ya Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwa mara ya kwanza msimu huu imefanikiwa kuhamisha wachezaji wake 10 na kupata nafasi zaidi za kusajili wachezaji wake nyota iliyowanasa katika usajili mdogo ambao unaendelea hivi sasa.


Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alisema hivi karibuni kuwa shirikisho hilo litakuwa makini katika kuhakikisha kuwa wachezaji wanaohamishwa wanakwenda katika timu za zinazoshiriki ligi kuu tu na pia ni lazima mchezaji husika akubaliane na uhamisho huo endapo atakuwa anasajiliwa na klabu inayoshiriki ligi ya chini.

Alisema kuwa katika zoezi la dirisha dogo timu ambazo hazikutimiza idadi ya wachezaji 30 katika usajili wa awali ndio zinazoruhusiwa kujaza nafasi hiyo kwa mujibu wa kanuni na zile ambazo zilitoa uhamisho wa nje.

Alisema kwa mujibu wa usajili uliofanywa awali, Azam FC ina nafasi tatu za kusajili wachezaji wapya lakini kufuatia kufanikiwa kufanya uhamisho sasa wana nafasi 10.

Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Fredrick Mwakalebela aliwataja wachezaji ambao Azam imefanikiwa kuwahamisha ni pamoja na Paul Nyangwe, Ally Alawi, John Mabula, Kassim Kilungo na Adamu Ngido ambao wanakwenda katika timu ya Manyema inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Ngazi ya Taifa.

Mwakalebela aliwataja wachezaji wengine kuwa ni pamoja na Yusuph Gogo, Mussa Kipawo, Zubeir Ubwa wanaokwenda Villa Squad ya jijini Dar es Salaam, Said Bakari na Abdulaziz Hamza wanakwenda Mkunguni.

Aliwataja wachezaji wapya wa hapa nchini walioombewa usajili kuwa ni Hahib Joseph ambaye ni huru, Nsa Job kutoka Polisi Morogoro na Ibrahim Mwaipopo wa Mtibwa Sugar.

Aliwataja wachezaji wanaotoka nje ya nchi ambao wameombewa vibali vya uhamisho katika nchi walizokuwa wanachezea kuwa ni pamoja na Dan Wagaluka (URA), Salvatory Ntebe (Vital`O), Francis Ouma (Mathare FC ya Kenya), Ibrahim Shikanda (Tusker FC), Maregesi Mwangwa (Fanja), Erasto Nyoni (Vital `O), Ben Karama (huru), Yasin Ahmed (huru), Chrispin Odula na Osborne Monday wa Tusker FC.

Pia Mwakalebela alisema kuwa TFF imetoa ITC kwa mchezaji, Erick Majaliwa wa Simba kwenda kucheza soka nje ya nchi huku pia James Chilapondwa wa Yanga akiombea ITC na klabu ya Bullet ya Malawi.

Aliongeza kuwa mabingwa watetezi wa soka Tanzania Bara, Yanga wameandika barua ya kumuombea ITC, Mike Baraza ambao pia wameonyesha nakala ya mkataba wa mwaka mmoja walioingia na mchezaji huyo huku Wachezaji wengine ni wapya walioombewa kusajiliwa ni wa timu ya JKT Ruvu ambao ni Abdallah Ngachiwa, Mwinyi Kazimoto na Damas Makwaya.

Zoezi la kukamilisha usajili wa dirisha dogo linatarajiwa kukamilika Novemba 30 na muda wa kuweka pingamizi ni kati ya Desemba Mosi hadi 15.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments