TIMU ya Soka ya Tanzania, Taifa Stars, imelipa kisasi kwa Msumbiji, Mambas baada ya kuilaza kwa bao 1-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika Uwanja Mkuu, Dar es Salaam jana.

TIMU ya Soka ya Tanzania, Taifa Stars, imelipa kisasi kwa Msumbiji, Mambas baada ya kuilaza kwa bao 1-0 katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki uliofanyika Uwanja Mkuu, Dar es Salaam jana.

Bao hilo la Kiggi Makassi aliyechukua nafasi ya Athuman Idd kipindi cha pili liliwainua vitini maelfu ya mashabiki waliofurika uwanjani hapo baada ya kutiwa kimiani katika dakika ya 79 ya mchezo huo, alipounganisha wavuni krosi ya Ngassa aliyefanya kazi kubwa ya kuihadaa ngome ya Msumbiji.

Katika mchezo huo, Stars ambayo ilishindwa kutawala sehemu ya katikati ya uwanja kipindi cha kwanza, walijikuta wakishindwa kuupitisha katikati na kulazimika kutumia winga ambako walikuwapo Mrisho Ngassa na Athuman Idd.

Lakini, walikosa nafasi kadhaa za wazi katika kipindi cha kwanza, kupitia kwa Jerry Tegete ambaye alishindwa kutumia krosi za Haruna Moshi ‘Boban’ na beki Shadrack Nsajigwa, aliyekuwa akisaidia mashambulizi.

Msumbiji, au Mambas waliitawala sehemu ya kiungo na katika dakika ya 30 na 44 walikaribia kuandika bao baada ya Dario Moteiro kumpasia mpira Goncalves Fumo, lakini shuti likatoka nje.

Nafasi nyingine kwa Stars ilikuwa katika dakika ya 45 kupitia kwa Ngassa aliyetumiwa krosi ya mbali na Boban akiwa na kipa Marcelino Cumbane aliyeshikwa na kigugumizi na kuutoa mpira nje.

Kipindi cha pili, Stars walianza kwa mabadiliko wakicheza kwa kasi, pasi za haraka haraka na dakika ya pili ya kipindi hicho Ngassa akaitoroka safu ya ulinzi ya Mambas na kumpa pasi Tegete, lakini akashindwa kumalizia wavuni mpira huo.

Dakika ya 61, Nsajigwa akapanda na kupangua safu ya mabeki wa Msumbiji na kuachia shuti kali ambalo lilipanguliwa na kipa na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.

Muda mfupi, Msumbiji wakajibu mapigo kwa Luis Muchue aliyepata pasi ya kisigino ya Tico Tico na kufyatua kombora ambalo lilitoka nje.

Baada ya mchezo, kocha Marcio Maximo alisema vijana wake wamejitahidi na walitarajia kuwa mechi ingekuwa ngumu na kwamba kutokana na ugumu huo, Msumbiji walitawala sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza ambacho hawakucheza vizuri ikilinganishwa na kile cha pili ambacho walipata bao.

Stars iliwakilishwa na Shaaban Dihile, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Nadir Haroub, Salum Swed, Godfrey Bonny, Mrisho Ngassa/Mgosi, Henry Joseph/Nurdin Bakari, Jerry Tegete/Nizar Khalfan, Haruna Moshi/Abdi Kassim na Athuman Idd/Kigi Makasi.

Mambas: Marcelino Cumbane, Antonio Gravata, Goncalves Fumo/Mohamed Hagi, Elias Pelembe, Manuel Bucuane ‘Ticotico’, Dario Monteiro/Luis Muche, Guilherme Manhique, Carlos Parruque, Francisco Massinga, Alimiro Lobo, Fanuel Massingue.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments