Mikataba TFF yafikia bil.4

Rais wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema kuwa katika uongozi wake ambao uliingia madarakani Desemba 27 mwaka 2004 wameweza kuingia mikataba mbalimbali yenye thamani ya Sh. bilioni nne jambo ambalo halikuwahi kutokea katika miaka ya nyuma.

Tenga katika taarifa yake ya utendaji ya miaka minne aliyoitoa jana alisema kuwa chini ya utawala wake mambo mbalimbali ya maendeleo yameweza kuboreshwa katika kiwango cha juu na kuweza kupata wadau wa kuisaidia katika nyanja tofauti za kukuza mchezo wa soka nchini.


Tenga aliyataja baadhi ya makampuni ambayo wameweza kuingia mikataba nayo na kiasi cha fedha wanachotoa kwa mwaka ni pamoja na Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) inayotoa zaidi ya Sh. milioni 700, Kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom (Sh. milioni 700), benki ya NMB (Sh. milioni 400), Coca cola (Sh. milioni 350) na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) inayotoa Sh, milioni 400 kwa ajili ya kudhamini mashindano ya Kombe la Taifa.

Pia TBL inatoa Sh. milioni 300 kwa ajili ya Kombe la Tusker, Sh. milioni 80 ( Kombe la Kagame) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kutoa Sh. milioni 100 za kukarabati ofisi za shirikisho hilo.

Alisema pia katika utawala wake timu ya taifa imeweza kupanda katika orodha ya ubora wa viwango vya Shirikisho la soka duniani (FIFA) kutoka nafasi ya 175 walipoikuta wakiingia madarakani na kuwa ya 105 hivi sasa.

Alisema katika uongozi wake wameweza kudhibiti fedha matumizi ya fedha kwa kuhakikisha kanuni za fedha zinazingatiwa kikamilifu na ukaguzi unafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi na wamepata hati safi ukaguzi kutoka kwa taasisi ya ukaguzi ya fedha inayotambuliwa na serikali.

Aliongeza kuwa katika kipindi cha kampeni si vyema wagombea wakaanza kulumbana na kutumia lugha zisizokuwa za kiungwana na wakati huu si wa kumpuuza mtu yoyote kwa sababu inawezekana ikapotezwa lulu inayohitajika katika ujenzi wa soka la nchi yetu.

Wakati huo huo, wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa TFF ambao umepangwa kufanyika Desemba 14 jijini Dar es Salaam juzi walidaiwa kupigana `vikumbo` mkoani Lindi kwa ajili ya kuendeleza kampeni zao za `chini kwa chini` ambapo mkoa huo ulikuwa unafanya uchaguzi wake katika mji wa Nyangao.

Pilika pilika hizo zilikuwa zinadaiwa kuwa ni maalumu kwa kuwasaidia wagombea waliokuwa wanawania nafasi za uongozi katika mkoa huo ili waweze kuja kuwapigia kura katika uchaguzi wa TFF.

Baadhi ya wagombea waliofika mkoani Lindi ni pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha soka Tanzania (FAT sasa TFF), Michael Wambura, aliyekuwa Katibu Mkuu wa klabu ya Yanga, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), Athumani Nyamlani.

Katika uchaguzi ujao wa TFF, Wambura na Nyamlani wanawania nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Malinzi anawania nafasi ya Urais.

Wakati huo huo, Shaibu Nampunde juzi alifanikiwa kutetea nafasi yake ya uenyekiti katika uchaguzi huo wa chama cha soka cha mkoa wa Lindi.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments