Rage sasa awania ujumbe TFF

Aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF, Ismail Aden Rage amejitosa kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji Kanda ya Magharibi katika Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 14 jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari jana, Rage alisema kuwa ameamua kuwania nafasi hiyo ili muda mwingine aweze kuutumia katika kuwaletea maendeleo ya soka wadau wa mkoa wa Tabora.

Rage aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa kilichokua Chama cha Soka Tanzania, FAT, kabla ya kuundwa kwa TFF, kwa sasa ni mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Tabora.

Hatahivyo, alisema kuwa mpira unatakiwa kuongozwa na watu wenye kujua fani ya soka ili kuleta msukumo ya kimaendeleo.

Rage anakuwa mgombea wa 10 kuchukua fomu kwa ajili ya kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

Wengine waliochukua fomu ni pamoja na Rais anayemaliza muda wake Leodger Tenga, Richard Lukumbula, Samuel Nyalla, Laurent Mwalusako, Shaibu Nampunde, Joseph Mapunda, Wailles Karia, Israel Mwaisasu na Eliud Mvela.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Makocha Tanzania, TAFCA, Sunday Kayuni amesema kuwa chama hicho kimeteua wajumbe wanne wa kamati ya uchaguzi watakaosimamia zoezi la uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 6.

Aliwataja walioteuliwa kuwa ni Ramadhan Mzee, Damas Ndumbaro, Juma Mwakemwa na Leslie Liunda.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments