Wageni wafurika Azam Fc

BENCHI la ufundi la Azam Fc limesema hakutakuwa na mapumzika kwa wachezaji wakati wa mapumziko ya Ligi Kuu na tayari wachezaji saba wa kigeni toka Uganda, Kenya na Msumbiji wameshawasili kufanya majaribio na kikosini hicho.

Azam ambayo ni msimu wake wa kwanza kushiriki Ligi Kuu ya Bara, haikufanya vizuri kwenye mzunguko wa kwanza uliomalizika hivi karibuni kwa madai kuwa hawakuwana muda wa maandalizi kabla ya ligi kuanza.

Kocha msaidizi wa timu hiyo, Sylvester Marsh aliiambia Mwananchi jana kuwa wachezaji saba wa kigeni tayari wameshatua kwenye timu hiyo na kuanza mazoezi lakini wiki ijayo watawatolea tamko.

“Sisi ni kama hatuna timu, hatukufanya vizuri sana kwenye mzunguko wa kwanza kwa vile muda wa maandalizi ulikuwa kidogo sana na ndio maana tumeamua kwamba hakuna likizo, tutawapa siku chache sana wiki zijazo,” alisema Marsh ambae aliwahi kuinoa Kagera Sugar kwa mafanikio.

“Tumeandaa programu nzito ambayo katika huu muda wote wa mapumziko timu itatengamaa vizuri, tayari Wakenya watatu, Msumbiji wawili na Waganda wawili wameshatua kwenye timu yetu.

“Rekodi zao zinaonyesha ni wachezaji wazuri, lakini tunawafanyia majaribio kwanza tuwaone mpaka wiki ijayo tutajua nini cha kufanya, hatujapata uhakika tuna nafasi ngapi za kujaza kwa vile kuna mambo yanaendelea kwenye uongozi,” alisema kocha huyo ambaye bosi wake ni Neider dos Santos wa Brazil.

“Kuna wachezaji tutawarudisha kwenye timu zao za daraja la kwanza, wengine tutawauza Ligi Kuu kuna makubaliano yanaendelea yakishamalizika ndio nafasi zao tutajaza muda si mrefu.”

Marsh ambae aliwahi kuinoa timu ya Taifa ya Vijana, Serengeti Boys alisema kiungo mshambuliaji wa APR ya Rwanda, Haruna Nyiyonzima anatazamiwa kutua nchini siku yoyote kuanzia leo huku Mganda, Danny Wagaluka wa URA wameshamalizana naye na amerudi kwao.

“Wagaluka tumeshamalizana naye na atarudi nchini siku si nyingi, kuna wageni wengine wataongezeka kwa majaribio pia siku si nyingi,”alisema kocha huyo ambaye timu yake imemaliza mzunguko wa kwanza ikiwa nafasi ya nane na pointi 13.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments