Yanga yamaliza uteja kwa Simba

UIMARA wa kipa Mzungu, Obren Curkovic, vurugu, imani za kishirikina na matukio yakiwamo ya mashabiki kurusha uwanjani chupa za maji ni baadhi ya matukio ambayo yalitawala mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyomaliza miaka karibu minane ya ubabe wa Simba dhidi ya Yanga.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa gumzo na ubishi mkubwa miongoni mwa mashabiki,Yanga imefaulu kushinda kwa bao 1-0 katika Uwanja Mkuu wa Taifa, Dar es Salaam.

Mchezo huo uliokuwa wenye ushindani, ufundi mkubwa ikilinganishwa na mechi zinazohusisha timu hizo, Yanga walipata bao, dakika ya 15 kupitia kwa Ben Mwalala baada ya kupokea pasi ya Boniface Ambani ambaye aliwatoroka mabeki wa Simba.

Utovu wa nidhamu hasa kwa wachezaji wa timu hizo mbili kwa kiasi kikubwa uliwasababishia kadi za njano zisizopungua tano na nyekundu tatu, nusura uharibu mchezo huo mkali na mtamu ambao ulikuwa wa kuvutia, ingawa mfungaji kinara wa ligi hiyo, Ambani alibanwa zaidi na walinzi wa Simba kiasi cha kubakia kivuli.

Mussa Hassan Mgosi, ambaye alitoka kifungo cha kusimamishwa na uongozi wa klabu hiyo siku chache kabla ya mchezo huo, aling’ara na kuwa kinara akisumbua ngome ya Yanga.

Mgosi huyo huyo, pia alikosa nafasi kadhaa za kuipa timu yake mabao, zikiwamo za dakika za 23, pia 33 za mchezo huo akiwa na kipa.

Dakika moja baadaye, nahodha Nico Nyagawa akakosa nafasi nyingine ya kuwapa Wekundu wa Msimbazi bao la kusawazisha.

Kipa Curkovic, raia wa Serbia langoni aliyecheza badala ya Juma Kaseja, kulikuwa ndiyo siri ama kichocheo cha Yanga kufanya vizuri akiendeleza rekodi yake ya kutofungwa, akiwa ameruhusu bao moja pekee.

Mzungu huyo, mara kadhaa alijitosa na kuokoa mashuti kadhaa ya washambuliaji wa Simba, hasa katika kipindi cha kwanza.

Mwamuzi wa mchezo huo, Victor Mwandike aliwaonyesha kadi za njano, beki Meshack Abel wa Simba na kiungo Athuman Idd ‘Chuji’ wa Yanga kwa mchezo mbaya.

Haruna Moshi alitolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi kwa kumpiga kibao Nadir Haroub Cannavaro akidai alikuwa amemchezea rafu ya kumrukia, jambo ambalo lilimkasirisha.

Dakika ya 76, mwamuzi aliwatoa nje kwa kadi nyekundu, Meshack Abel na Mwalala baada ya kutishiana kuzipiga ngumi.

Kipindi hicho, Simba iliwatoa Gabriel na Nyagawa na kuwaingiza Ulimboka Mwakingwe na Mohammed Kijuso.

Yanga nao waliwapumzisha Ngassa na Chuji na kuingia Castory Mumbala na Kigi Makassy.

Hata hivyo, Mwandike alimpa kadi ya njano, Emmanuel Gabriel kwa kujiangusha kwa makusudi katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo.

MATUKIO

Simba waliingia uwanjani muda wa saa 8.45 mchana kwa mbwembwe huku Mgosi akiwa wa kwanza kushuka kutoka katika gari aliingia uwanjani akifuatwa na mwenyekiti, Hassan Dalali.

Wawili hao walikwenda hadi kona ya kaskazini mwa uwanja wakifuatwa na kundi zima la wachezaji, wanachama wa kundi la Friends of Simba ambao wanataka kuingia uwanjani, lakini wakazuiwa na wanausalama.

Yanga kwa upande wao waliingia uwanjani saa 9.00 wakiongozwa na winga Mrisho Ngassa na kwenda hadi katikati ya uwanja, akainama na kushikana paji la uso akifuatiwa na wenzake.

Katika kipindi cha kwanza, mashabiki wa Simba wanataharuki na kuanza kurusha chupa za maji uwanjani wakipinga kitendo cha mwamuzi Mwandike kupeta baada ya wachezaji wao watatu kufanyiwa madhambi.

Nje ya dimba, mashabiki nao walijaribu mara kadhaa kurushiana ngumi za hapa na pale, ingawa askari walikuwa macho kutuliza rbasha hizo ikiwamo kutumia mabomu ya machozi kutawanya mashabiki waliojaribu kuingia uwanjani uliokuwa umesheheni mashabiki na tiketi kumalizika.

Matukio ya imani za kishirikina nayo pia yalichukua sehemu ya mchezo huo baada ya Mgosi, dakika ya 69 kwenda katika lango la Yanga, kufukua na kuondoka na kitu kinachodaiwa kuwa hirizi.

Mgosi alitupa kitu hicho nje ya uwanja ambako shabiki mmoja alikiokota na kwenda nacho upande walikokuwa mashabiki wa Simba.

Kitendo hicho kilimzawadia kadi ya njano Mgosi. Tukio hilo linachafua hali ya hewa uwanjani kwa wachezaji kuonyeshana ubabe, kurushiana ngumi.

Mashabiki wa Simba wanafanya vurugu zikiwamo za kurusha chupa za maji kuelekea kwa wachezaji wa Yanga na mwamuzi huyo huku wakimlaumu kuwa aliwabeba kwa kiasi kikubwa wapinzani wao.

Mwakingwe, ambaye aliifunga Yanga mwaka jana katika Ligi Ndogo aliangua kilio baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi huyo.

Kwa upande wa Yanga ni nderemo, vifijo na nyimbo mbalimbali zikieleza kuwa zama za uteja kwa Simba basi!

Kocha wa Yanga, Dusan Kondic alieleza kufurahishwa na mchezo,pia matokeo akieleza kuwa ameibadili historia mbaya ya timu yake kufungwa na Simba.

Alieleza kuwa ushindi huo umechangiwa na wachezaji wake ambao walicheza bila shinikizo.

Mwenzake wa Simba, Krasimir Bezinski alieleza kuwa timu yake imecheza vizuri kuliko Yanga, lakini washambuliaji wake ndio waliomwangusha kwa kukosa umakini.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments