Mashabiki wa soka Tanzania washangazwa na ubora wa Taifa Star

Kiungo wa Taifa Stars Athuman Idd aka Chuji ambaye alifunga moja ya mabao kwa kisigino akichuana na mchezaji wa Cape Verde katika pambano ambalo Taifa Stars walishinda kwa 3-1 jijini Dar, Jumamosi

SIJUI walikuwa wapi…wanakumbuka shuka kumekucha…Stars imekipiga sana leo… ni kauli za mashabiki baada ya mchezo kati ya Taifa Stars na Cape Verde ambao ulimalizika kwa wenyeji kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 katika mchezo mkali kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa.

Taifa Stars ambayo haikuwa na nafasi, ilichokuwa imekifanya ni kuiharibia Cape Verde isifuzu pamoja na kujitengenezea mazingira ya kupanda kwa ubora katika ngazi za Shirikisho la Soka la Kimataifa, FIFA.

Matokeo hayo yameifanya Stars kufikisha pointi inane na kushika nafasi ya tatu huku Cape Verde ikishika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi tisa. Cameroon iliyokata tiketi, ilikuwa ikicheza na Mauritius jana.

Walikuwa Athumani Idd ‘Chuji’, Jerson Tegete na Mrisho Ngassa waliokuwa mashujaa wa mchezo huo kwa kuzifumania nyavu za Cape Verde ambao walishinda mchezo wa kwanza kwa bao 1-0.

Ikicheza kwa kujiamini, Stars ilianza kuzitikisa nyavu za wapinzani wao katika dakika ya tano kwa bao la Chuji ambaye alilifunga kwa kisigino baada ya kupiga shuti mara mbili na mpira kumrudia, na aliposhindwa kugeuka, aliupiga kwa kisigino na kumpita kipa Soarese Ernesto.

Stars waliongeza mashambulizi huku Ngassa akiwa burudani uwanjani kutokana na soka yake, na dakika mbili baada ya bao hilo, Tegete alikosa bao la wazi baada ya kupata pasi ya Henry Joseph aliyepokea mpira wa Ngassa.

Dakika ya 18, Haruna Moshi ‘Boban’ alitoa pande murua kwa Tegete lakini alipoteza. Hata hivyo alisahihisha makosa yake na kufunga katika dakika ya 26 baada ya kumtoka beki wa Cape Verde, Neves Fenando.

Boban aliyesimama imara katika nafasi ya kiungo mshambuliaji, alimjaribu kipa Soanes dakika ya 32 lakini shuti lake alilitoa na kupeleka mashambulizi langoni kwa Stars, mpira uliozaa bao dakika ya 34. Alikuwa Semedo Jose aliyetumia makosa ya kukatika kwa ngome ya Stars na kuwapiga chenga Shadrack Nsajigwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.

Kipindi cha pili, kocha wa Stars Marcio Maximo alifanya mabadiliko kadhaa yaliyoipa nguvu Stars, na katika dakika ya 65 na 68 Boban alitoa mipira safi ya krosi lakini hakukuwa na mmaliziaji.

Dakika ya 74, Juma Jabu alipanda na mpira kuanzia katikati ya uwanja na kutoa pasi kwa Ngassa ambaye naye alimuita kipa wa Cape Verde na kumvisha kanzu iliyokwenda moja kwa moja kimiani. Lilikuwa bao tamu lililoshangiliwa na uwanja mzima.

Kocha wa Cape Verde, Joao Deus aliikubali soka ya Taifa Stars na kusema: “Tanzania imecheza vizuri, sikutegemea kama wangecheza soka namna hii…leo ilikuwa siku yao. Nasema tumefungwa kutokana na uchovu wa safari ndefu lakini bado nasema Tanzania leo imecheza mpira.

“Nasikitika tumepoteza matumaini ya kusonga mbele, tulitaraji kushinda lakini matumaini hayapo tena, ispokuwa nasema, Sudan wana kazi, hii inatoa mwanga kuwa mtafika mbali .”

Naye Maximo aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi na kusema: “Nimefurahi tumeshinda na huu ushindi ni heshima kwa Watanzania. Wachezaji wangu wametengeneza nafasi nyingi za kufunga na nashukuru wamezitumia.

“Nilipanga timu nyingine kwa kuwatumia wachezaji wapya kikosini, Nurdin Bakari na Haruna Moshi, lakini nashukuru wamecheza vema.”

Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, George Mkuchika naye alisema: “Nilifanya kazi ya kuwapa nguvu, hii ni changamoto kubwa kwani sasa tuna mechi ngumu na Sudan, lazima tufanye kazi kushinda.”

Stars iliwakilishwa: Ivo Mapunda, Shadrack Nsajigwa, Juma Jabu, Salum Sued, Nadir Haroub, Nurdin Bakari, Henry Joseph/Jabir Aaziz, Haruna Moshi/Kiggi Makasi, Jerry Tegete/Mussa Hassan Mgosi, Mrisho Ngassa na Athumani Idd.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments