JK aishukuru China kwa uwanja

Rais Jakaya Kikwete ameishukuru serikali ya China kwa ujenzi wa uwanja wa kisasa wa michezo jijini, Dar es Salaam.

Akizungumza na ujumbe wa Chama cha Kikomunisti cha China ulioongozwa na He Yong jana, Kikwete aliomba shukrani hizo zifikishwe kwa Rais wa China, Hu Jintao.


“Tunawashukuru sana kwa uwanja,“ alisema Kikwete kwenye mazungumzo yaliyofanyika kwenye uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Yong, ambaye ni Katibu wa Sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China, aliongoza ujumbe wa chama hicho uliokuwa na ziara kwa mwaliko wa Chama cha Mapinduzi.

Ziara hiyo ya ujumbe wa China ilikuwa sehemu yao ya ziara katika nchi za Afrika. Walitembelea nchi za Afrika Kusini, Uganda, Gabon na Nigeria.

Rais Kikwete alisema uwanja huo umevutia hata Shirikisho la soka la Kimataifa (FIFA) na kudokeza kuna uwezekano kwa baadhi ya nchi zitakazoshiriki fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010 nchini Afrika Kusini kutumia uwanja huo kwa maandalizi.

“Mwambie Rais Jintao kuwa tunashukuru sana kwa kutuunga mkono kwa hilo. Asanteni sana kwa urafiki wenu wa kindugu,“ aliongeza Rais Kikwete.

Yong naye aliahidi atawasilisha shukrani hizo za Rais Kikwete na kuongeza kuwa Wachina wamekuwa wakifurahia uhusiano uliopo wa kindugu ulioanza miaka 44 iliyopita.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments