TFF kujadili miaka minne ya utawala wao

SHIRIKISHO la Soka Tanzania, TFF, limeanza harakati za kujiandaa na mkutano mkuu mwezi Desemba na sasa limeandaa kongamano la siku tatu kwa wadau wa soka kuzungumzia mkutano huo..

Mkutano mkuu wa shirikisho hilo utafanyika mapema mwezi Desemba ukifuatiwa na uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo chini ya uongozi wa Leodegar Tenga na Makamu wake, Crescentius Magori unamaliza muda wake.

Uongozi huo wa Tenga uliingia madarakani Desemba 28, 2004 na tayari vuguvugu kwa ajili ya uchaguzi huo limeanza kufukuta huku aliyekuwa katibu mkuu wa shirikisho hilo ambaye aliangushwa na Tenga kwenye uchaguzi wa mwaka 2004 Michael Wambura kukiwa na tetesi kuwa atawania nafasi ya juu kwenye uchaguzi huo wa Desemba.

Likiwa linajipanga kwa ajili ya uchaguzi huo, shirikisho hilo limeandaa Kongamano kwa wadau wa soka ambalo litafayika Septemba 18 hadi 20 kwenye Ukumbi wa NSSF Water Front jijini Dar es Salaam.

Kongamano hilo ambalo limeandaliwa na TFF kwa kushirikiana na Chama cha Makocha Tanzania (TAFCA), lina lengo la kutathmini mwenendo mzima wa soka ya Tanzania tangu uongozi wa Tenga ulipoingia madarakani mpaka hivi sasa.

Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema kongamano hilo litakuwa la kitaifa na litakalotoa nafasi kwa wadau kutoa maoni yao ya nini kifanyike ili kukuza na kuendeleza soka ya Tanzania.

“Kongamano hili litaeleza nafasi ya makocha, waamuzi na madaktari wa michezo katika maendeleo ya soka,” alisema Mwakalebela.

Alisema: ”TFF pia tutaweka wazi matarajio yetu masuala mazima ya fedha, na vyanzo mbali mbali vinavyotuingizia pesa ikiwa ni pamoja na mikakati yetu katika kuhakikisha TFF inajiwezesha yenyewe katika masuala mazima ya fedha pamoja na miundo mbinu kwa maana ya viwanja.”

Kongamano hilo limepangwa kufunguliwa na Naibu Waziri wa Habari na Utamaduni Joel Bendera na litafungwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Idd Kipingu.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments