Taifa Stars ilipokumbuka shuka kumekucha

MAGOLI manne yaliyofungwa katika kipindi cha kwanza na Kigi Makasi, Nizar Khalfan na Jerson Tegete aliyefunga mawili, yalitosha kuipa Taifa Stars ushindi mnono wa magoli 4-1 dhidi ya Mauritius katika mechi ya kukamilisha ratiba ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia na Afrika iliyofanyika kwenye mji wa Port Louis.

Huo ni ushindi wa kwanza mkubwa wa ugenini katika historia ya Taifa Stars katika michuano ya CAF na FIFA na ndiyo ushindi wa magoli mengi tangu mwalimu Marcio Marcio Maximo aaanze kuinoa timu hiyo miezi 25 iliyopita huku ukiwa ushindi wa pili wa ugenini kwa Maximo tangu alipoilaza Burkina Faso kwa 1-0 mjini Ouagadougou Juni 16, 2007 kwa goli la mlinzi Erasto Nyoni.

Kabla ya mchezo huo, ushindi mkubwa wa ugenini uliokuwa ukishikilia rekodi kwa Taifa Stars ni ule wa magoli 3-1 dhidi ya Uganda Cranes uliopatikana kwenye Uwanja wa Nakivubo mwaka 1984, huku ushindi mkubwa kabisa kwa michezo yote ya nyumbani na ugenini ya CAF na FIFA ukibakia kuwa wa magoli 5-0 dhidi ya Kenya mwaka 1979 jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mfalme George V katika Manispaa ya Curepipe, Stars iliyoonekana kuwa na shauku kubwa ya kulinda heshima ya Tanzania ilianza biashara mapema kwa kuandika goli la kwanza katika dakika ya 11 kupitia kwa kiungo wa kushoto Kigi Makasi kwa mpira wa adhabu ndogo uliokwenda moja kwa moja nyavuni. Adhabu hiyo iliamuliwa ipigwe na mwamuzi Alfred Ndinya wa Kenya baada ya Mrisho Ngassa kufanyiwa madhambi.

Hilo lilikuwa goli la kwanza la kimataifa kwa Makasi ambaye alikuwa anafurahia kupangwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha kwanza cha wachezaji 11. Furaha yake ilioekaa dhahiri pale aliposhangilia kwa kubiringika hewani katika mtindo wa sarakasi.

Kuingia kwa goli hilo kulikuwa kama vile kumewafanya Mauritius waamke usingizini na kufaya mashambulizi mawili ya nguvu na kufanikiwa kusawazisha dakika mbili tu baadaye kupitia kwa Wesley Marquette aliyeujaza mpira wavuni kwa tick-tack.

Hata hivyo, bao hilo halikuwachanganya wachezaji wa Taifa Stars na waliendelea kulishambulia lango la wapinzani kama nyuki. Jitihada hizo zilizaa matunda katika dakika ya 19 wakati kiungo mahiri Nizar Khalfan alipoukwamisha mpira ndani ya kimia ikiwa ni bao lake la saba la kimataifa.

Nizar alipokea mpira mrefu uliopigwa na Shaaban Nditi kutoka wingi ya kulia naye akiwa ndani ya eneo la hatari aliumiliki vema kabla ya kuachia shuti la chini na kuifugia timu yake goli la pili.

Kuanzia hapo Stars walianza kucheza watakavyo na kuwabana vilivyo wapinzani wao na kufanikiwa kuandika goli la tatu kupitia kwa Jerson Tegete katika dakika ya 23.

Tegete, mmoja wa wachezaji vijana walionolewa na kocha Maximo na hatimaye kupewa jukumu la kuvaa jezi namba 10, huku akipangwa kwa mara ya kwanza kuanza katika mchezo wa kimashindano, alifunga goli maridadi akipokea pasi ya safi ya Nizar Khalfan.

Tegete aliendelea kudhihirisha kuwa Maximo hakukosea kumwamini kumpatia nafasi hiyo muhimu ya kuongoza safu ya ushanbuliaji ya Stars, pale alipofunga goli la nne dakika tano baadaye yaani katika dakika ya 28 pale alipomalizia kazi maridadi iliyofanywa na Ngassa.

Ngassa alikimbia na mpira pembeni kulia na kuachia krosi murua ambayo Tegete hakupata kazi kubwa kumtungua mlinda mlango Ammomoothoo wa Mauritius. Hadi mapunmziko Stars ilikuwa mbele kwa magoli 4-1

Mauritius ilikianza kipindi cha pili kwa kasi huku ikionesha dhamira ya kusawazisha mabao lakini ngome ya Taifa Stars ilikuwa imara chini ya Nadir Haroub ‘Cannvaro’.

Kocha Maximo alifanya mabadiliko katika kipindi hicho kwa kumwingiza Mussa Hassan Mgosi badala ya Kigi Makasi katika dakika ya 59, Adam Kingwande naye aliingia badala ya Tegete katika ya 74 huku Jabir Aziz akichukua nafasi ya Nditi katika dakika ya 80.

Mabadiliko hayo yaliweweza kuifanya Stars iendelee kutawala sehemu ya kiungo na kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara katika lango la Mauritius lakini hakukuwa na mabadiliko.

Mgosi angeweza kufunga katika dakika ya 63, dakika nne tu baada ya kuingia uwanjani pale alipoachia kombora kali lakini golikipa wa Mauritius alipangua na kuwa kona tasa.

Dakika tatu kabla ya hapo nusura Mauritius wafunnge goli pili pale mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Louis Cundasamy ulipogonga mwamba wa juu na kutoka nje.

Na katika dakika ya 87 golikipa Ivo Mapunda alifanya kazi ya ziada kupangua shuti kali la Andy Sophie aliyekuwa ametazamaa naye na baadaye mpira kuokolewa na walinzi wa Stars.

Mwamuzi Alfred Ndinya wa Kenya alitoa kadi moja tu nya njano kwa kiungo Geofrey Bonny wa Stars.

Baada ya mchezo huo kocha Maximo alisema kuwa amefurahishwa na matokeo ya mchezo hasa ikizingatiwa kuwa mchezo ulikuwa ni wa ugenini.

Ameeleza kuwa sasa ni wazi kikosi chake kimeweza kuiva na matunda ya kuwaandaa vijana kam vile Tegete, Ngasa, Juma Jabu Makasi Nizar na wengineo yanaanza kuoekana.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments