Tanzania kuivaa Mauritius ili kulinda heshima

TAIFA Stars leo itakuwa ikicheza mechi yake ya kwanza ‘bila ya presha’ wakati itakapoivaa Mauritius jijini Port Louis, ikiwania zaidi kulinda heshima na kujenga jina baada mechi nne za kwanza kushindwa kuijengea msingi wa kwenda Afrika Kusini na Angola.

Stars, inayofundishwa na Mbrazili Marcio Maximo ilionyesha soka la hali ya juu kwenye mechi hizo nne za kwanza za michuano ya awali ya Kombe la Dunia/Mataifa ya Afrika, lakini sare dhidi ya Mauritius jijini Dar es salaam na vipigo vya ugenini dhidi ya Cape Verde na Cameroon vilifuta ndoto za kufuzu kucheza fainali hizo.

Stars ilitengeneza nafasi nyingi katika mechi ya kwanza dhidi ya Mauritius, lakini ikaambulia bao moja lililoipa sare ya bao 1-1 na wageni hao na baadaye kukubali kipigo cha bao 1-0 ugenini mbele ya Ivory Coast kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Cameroon jijini Yaounde katika mechi ambayo Stars ilionyesha kukomaa.

Matokeo hayo pamoja na sare ya bila kufungana dhidi ya Cameroon kwenye Uwanja wa Taifa yaliinyima Stars tiketi ya kwenda Afrika Kusini kwenye fainali za Kombe la Dunia, na Angola kwenye fainali za Mataifa ya Afrika, zote zikifanyika mwaka 2010.

Kwa maana hiyo, Stars itakuwa inaingia uwanjani ikiwa haina wasiwasi wowote mbele ya Mauritius, ambao pia hawana matumaini yoyote ya kwenda mbele baada ya kupoteza mechi tatu isipokuwa ile ya Stars.

Pengine matatizo pekee yanayoweza kuiathiri timu ni kitendo cha upekuzi uliokithiri kwa baadhi ya viongozi alioambatana na timu, kitu ambacho hakiwezi kuingia akilini mwa wachezaji na kuwaathiri.

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka (TFF), Florian Kaijage alisema mara baada ya kutua kwenye Uwanja wa ndege wa kimataifa Port Louis, walifanyiwa upekuzi mkubwa isivyo kawaida.

“Tulipekuliwa kila kitu na maafisa wa uhamiaji na askari. Hii ilitupa wasiwasi sana kwa kuwa hatukujua ni kwa nini,” alisema.

“Sijui sana ni jinsi gani wanafanya kazi lakini, sisi tu ndio tulipekuliwa na wasafiri wengine waliachwa wakaenda zao.”

Ukiachana na mambo hayo, Maximo atakuwa akitegemea washambuliaji wake kujisahihisha baada ya kuichambua ngome ya Mauritius kila mara katika mechi ya Dar es salaam, lakini wakashindwa kumtungua kipa.

Emmanuel Gabriel, ambaye hajachezeshwa tangu ashindwe kutikisa nyavu katika mechi hiyo na ile ya Cape Verde.

Danny Mrwanda na Mrisho Ngassa ndio walioongoza safu ya ushambuliaji katika mechi zilizofuata, lakini Mrwanda hatakuwepo leo na badala yake Jerry Tegete ataanza pamoja na pamoja na Ngassa kusaka mabao ya heshima.

Nizar Khalfan ataongoza kiungo kusaidia washambuliaji hao akiwa pamoja na Kigi Makasi (kushoto) na Shaaban Nditi (kulia) huku katikati yao akicheza Godfrey Bonny, ambaye amekuwa akifanya kazi kubwa ya kupokonya mipira na kuituliza timu.

Huu ni mchezo muhimu kwa timu hiyo ili kuweka matumaini kwa mashabiki baada ya kukosa tiketi ya Afrika Kusini na Angola.”Tutacheza kufa na kupona.

Hali ni nzuri kwa kila mchezaji; nia yetu ni pointi tatu na sio moja au kukosa kabisa, tuna imani kuwa tunaweza kufanya vizuri ingawa tunapambana na timu ngumu,” alisema Maximo aliyeiongoza Stars katika michezo 27 kwa kipindi cha miaka miwili.

“Hii ni moja ya maandalizi yetu ya mchezo mgumu dhidi ya Sudan. Tutacheza kufa na kupona na hapana shaka kuwa tutafanya vizuri.”

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments