Tunasibiri majaliwa ya Kikwete katika riadha Tanzania

ALHAMISI Agosti 21, 2008, Rais Jakaya Kikwete alizungumza na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu masuala mbalimbali yanayolikabili Taifa.

Wengi walikuwa wakitega masikio kusikiliza nini atakisema. Kati ya yote aliyosema, wengi walikuwa wakitaka eneo la waliokwapua mafedha ya wananchi katika fuko la EPA. Hapa ndipo wengi walipokuwa wanasubiri kwa hamu.

Lakini pamoja na yote, kwa hayo aliyoyasema, mwisho wa siku akawapa waliokomba fedha za EPA kuyarudisha hadi Oktoba 31.

Kimsingi, hatuangalii sana huko kwa akina EPA, zaidi ya kuangalia eneo moja la hawa watu wa riadha.

Baada ya kuwapasha Shirikisho la Soka Tanzania, TFF kuwa wakati umefika sasa wasake fedha kwa ajili ya kuwalipa makocha, Rais Kikwete akasema, baada ya kumalizana na TFF ataingia katika riadha.

Tayari Katibu Mkuu wa RT, Suleiman Nyambui amesema kauli ya rais aliyoitoa mjini Dodoma  inalenga katika kuinua kiwango cha mchezo huo siku za usoni

Alisema wanatarajia kulifikisha suala hilo kwenye kamati ya ufundi, baadaye kwenye kamati ya utendaji kabla ya kujadiliana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ili wafikie uamuzi.

Kwanza, kauli ya Nyambui ni kama ya kujikosha kwa kuwa inaonekana wameshindwa kuleta mabadiliko katika chama hicho.

Wakati wanafanya uchaguzi wa Julai, 2006 huko Mwanza viongozi waliochaguliwa, walipania kuendeleza mchezo huo ambao sehemu kubwa unachezwa Dar es salaam, Zanzibar, Arusha, Singida na Manyara.

Jukumu kubwa ambalo liliwapasa kuwa nalo wahusika, ni kuhakikisha AT inakuwa na matawi Tanzania, na kuendeleza riadha kitaifa, lakini hilo halipo.

AT wamekalia kugombana na TOC juu ya wadhamini, lakini nenda Ruvuma, nenda Mikindani Mtwara, nenda Kagera, AT wanaweza kusimama na kusema katika kipindi cha miaka miwli tangu kuingia madarakani riadha imesimama?

Nani anayeweza kuthubutu? Leo hii tunaambiwa kuna mashindano ya taifa, hatujaisikia Rukwa, Kigoma ndiyo mwaka huu imeshiriki kwa mara ya kwanza na wengine hakuna kitu.

Kingine cha kusikitisha, AT wanashindwa vipi kutengeneza vijana kwa mbio za mita 100, 200, 800, 1500 na hata 400 Relay? Kwa walioangalia Michezo ya Olimpiki, Beijing inatia uchungu. Dunia ilikuwa imejiandaa katika maeneo hayo.

AT inashindwa vipi kuwapata warusha mkuki, kutupa kisahani, kurusha tufe, kuruka chini, kuruka juu, kuruka viunzi?

Tumeshuhudia Michezo ya Olimpiki ya Beijing iliyomalizika Jumapili Agosti 24, kweli ukiangalia timu ya Tanzania unaweza hata kutoa machozi.

Haya, tukasema tunapeleka mita 5000, 10,000, 8000 na marathon, angalia matokeo, angalia nafasi walizomaliza wanamichezo hao wa Tanzania.

Itakumbukwa, katika mbio za mita 5000, Mtanzania alishika nafasi ya mwisho, wenzake wanakimbia yeye ananyata, hakika kila Mtanzania alimshangaa na hata kujiuliza, hawa walifuzu vipi michezo hii.

Inasikitisha kweli kuona Tanzania inafanya vibaya katika riadha na michezo ya uwanjani. Haiwezekani kuendelea kutegemea riadha kwa marathon na hiyo marathon yenyewe ndiyo hiyo Mtanzania wa kwanza kashika nafasi ya 55, kweli inatia uchungu!?

Kufuzu kwao kwa michezo ya Olimpiki kunatia shaka. Siku ya kwanza tulipoteza medali za akina Dickson Marwa na Fabian Joseph ambao walichemsha katika mbio za mita 5000 kirahisi mno.

Tulimtarajia Zakia Mrisho katika mita 5,000 naye akaibuka nafasi za mbali kabisa, hata hakufurukuta.

Samuel Mwera naye kavurunda mita 800 akiwa wa mwisho wakati Fabian Joseph alipoteza medali nyingine ya mita 5,000.

Tukawa na matumaini kwa akina Samson Ramadhani, na Getuli Bayo na Msenduki Mohamed kwa marathon.

Mohamed hakukimbia ni kama kenda kutalii, lakini tunaona mkimbiaji wa kwanza Tanzania, Samson Ramadhani amekuwa wa 55. Hapa kuna masihara sana.

Tanzania ilipata medali za Olimpiki mara ya mwisho 1980 baada ya wanariadha wake, Filbert Bayi na Suleiman Nyambui kushika nafasi za pili katika mbio za mita 3,000 na 5,000. Michezo hiyo ilifanyika kwenye mji wa Moscow.

Ni aibu. Ingia kwenye chama mheshimiwa kwa kuanmza kukifumua. Pamoja na kwamba tutasema yapo mataifa nayo yametoka kapa, sasa kwanini tuangalie wenzetu, hapa tunajiangalia sisi.

Kenya wameweza vipi kuondoka na dhahabu tano za Olimpiki? AT wanashindwa vipi kupokea mafunzo na mbinu za Wakenya? Kwanini wanamichezo wasiende kujifunza Ethiopia?

Wakati wa JK kuingia kwenye kapu la AT, naamini kuna mengi atakutana nayo huko.

Cha kwanza cha kujiuliza, Je AT kuna program endelevu? Kuna shule ngapi za riadha? Tunadhani AT wanaangalia kwa uzoefu kuwa mikoa ya Manyara, Arusha na Singida kama ndiyo shule za riadha, sivyo, kuna mipango inatakiwa kufanyika.

Mpaka sasa ni miaka 28, na baada ya Olimpiki ya Beijing ni miaka 29 Tanzania haijawahi kutwaa hata shaba katika michezo hiyo ya Olimpiki.

Baada ya kuipika upya AT, tunataka kuona mafanikio katika michezo ya Madola India 2010, Michezo ya Afrika, Lusaka 2011 na Michezo ya Olimpiki 2012 London.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments