Thadeo awaonya wanaokwenda China

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa,(BMT), Leonard Thadeo amewaasa wanamichezo wa Tanzania wanaokwenda nchini China kushiriki michezo ya Olimpiki inayotarajia kuanza Agosti 8 kutoliingiza Taifa kwenye kashfa ya kubeba madawa ya kulevya.

Thadeo, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akipokea vifaa vya michezo kwa ajili ya wanamichezo hao vilivyotolewa na Kampuni ya kitengo cha makontena (TICTS).

Alisema kuwa kila Mtanzania anajua kuwa katika kipindi hiki nyanja ya michezo imekumbwa na sakata zito hasa baada ya timu ya taifa ya ngumi kutuhumiwa kubeba madawa ya kulevya nchini Mauritius, ilipokuwa imekwenda kwenye michezo ya ngumi ya Afrika.

“Jamani nafikiri sisi wote tunayo taarifa ambayo si nzuri kwenye upande wetu wa michezo, kashfa iliyopo ni kubwa hivyo nawaomba ndugu zangu mnaokwenda China kuacha kubeba vitu visivyohusika na michezo hiyo, tafadhali msithubutu kufanya hivyo,“ alisema Thadeo.

Thadeo, aliwataka wanamichezo hao kuacha tamaa kwa kufanya vitu vya ajabu, ambapo pia aliwataka kuacha kutumia madawa ya kuongeza nguvu kwenye michezo hiyo na zaidi aliwataka kuhakikisha kuwa wanatumia vema mafunzo waliyopewa ili kurudi na medali nchini.

Kwa upande wake mwakilishi wa TICTS, Cassian Ng’amilo alisema kuwa kampuni yao itaendelea kuidhamini timu hiyo, ambapo alisema watakapokuwa nchini China watakuwa karibu na makao makuu ya kampuni hiyo hivyo wataendelea kupatiwa uangalizi wa kutosha.

Aliwataka wanamichezo hao kuhakikisha wanajituma ili kurudi na medali hapa nchini,ambapo Kocha wa timu ya riadha, Juma Ikangaa alisema kuwa wana imani ya kurudi na medali.

Wanamichezo wanaoondoka keshokutwa kwa upande wa wanariadha ni Zakaria Mrisho, Samson Ramadhani, Msenduki Mohamed, Getuli Bayo, Dickson Marwa, Samwel Kwaang`w, Samwel Mwera na Fabian Joseph, waogeleaji ni Khalid Rushaka na Magdalena Moshi.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments