Manji Yanga-damu au anataka damu ya Yanga?

KWA mwanayanga yeyote, ni lazima atakuwa anatembea kifua mbele kutambia usajili wa kufuru uliofanywa na bilionea kijana mwenye umri wa miaka 30 tu! Yusuf Mehboob Manji.

Kwa hakika, Manji ameitikisa nchi kwa usajili wake wa msimu wa 2008/9, baada a kusajili kikosi chenye thamani ya shilingi milioni 500 na ushee.

Inaelezwa kwamba, licha ya kumfanya kipa Juma Kaseja avunje rekodi ya usajili Afrika Mashariki na Kati kutokana na kunyakuliwa kwa dau la zaidi ya shilingi milioni 75, mchezaji aliyelamba fedha kidogo kabisa katika usajili, hakukosa shilingi milioni 8..

Manji amekwenda mbali zaidi na kumsajili kipa kutoka Ulaya, huko Serbia kwa zaidi a shilingi milioni 130!

Nyota hao wote kutoka nchi mbalimbali za Afrika na Ulaya, wakiwamo wengi wa timu ya soka ya Tanzania `Taifa Stars’, kwa ujumla wameandika historia.

Na Manji ameandika historia ambayo bado ni gumzo katika soka ya Tanzania, kila mmoja akihoji ilikotoka jeuri hiyo ya usajili.

Mbali ya kukusanya nyota wanaoaminia kuwa na vipaji halisi vya soka, Manji ameipa pia Yanga timu ya makocha watatu, wote kutoka Ulaya.

Pamoja na usajili na mambo mengine kadha wa kadha makubwa anayoifanyia Yanga, Manji kwa sasa ndiye baba, akiitunza timu kwa takribani shilingi milioni 2.5 kwa siku katika hoteli ya Lamada, Ilala jijijini Dar es Salaam.

Kiasi hicho cha fedha wastani wa sh milioni 75 kwa mwezi, achilia mbali mishahara na madudu mengine ya kila aina.

Kwa kifupi, viongozi wa Yanga hawapasui kichwa hata chembe juu ya uendeshaji wa timu, mishahara, safari, malazi na mambo mengine. Wameridhika na kudiriki kutembea kifua mbele kwamba hakuna linaloishinda Yanga, kama jambo husika litahusiana na masuala ya fedha.

Pamoja na kumshukuru Manji na kutambia fedha zake, bado kuna maswali lukuki ya kujiuliza.

Kwa mfano, wakati anatia mguuu Jangwani na kupokelewa kwa kila aina ya nderemo, Manji aliahidi kuikomboa klabu kiuchumi.

Akaanza mbwembwe za kupeleka seti ya televisheni klabuni ili wanachama wawe wanakutana hapo na kubadilishana mawazo. Akahamishia nguvu kwenye kuukarabati Uwanja wa Kaunda unaomilikiwa na klabu hiyo. Tukashuhudia makatapila akichimbua uwanja, lakini ghafla tukashuhudia udongo uliochimbuliwa ukigeuka tope kutokana na mvua kubwa mfululizo.

Mpaka leo hakuna kilichoendelea, zaidi ya kusikia malumbano ya hapa na pale na aliyekuwa mweka hazina, Abeid Abeid `Falcon’.

Na hata klabuni, hakuna kilichoendelea. Jengo la Yanga ghorofa tatu limebaki kuwa gofu, ingawa makadirio ya ukarabati wake, ikiwa pamoja na vyumba takribani 20 vya wachezaji, vingeweza kula si zaidi ya sh milioni 150.

Hii ina maana kwamba, klabu ingerudisha hadhi na hata kuifanya iwe na kambi ya kudumu klabuni hapo, huku sehemu nyingine za klabu zikitumika kama vitegauchumi, achilia mbali jengo la Mtaa wa Mafia linalozidi kufanana na banda, licha ya kuwa katika eneo zuri kibiashara.

Kukamilika kwa ukarabati wa jengo kungeweza kuisaidi mno Yanga katika kuepuka gharama za kuwapangishia nyumba wachezaji `wasela’, gharama za kambi na mambo mengi kadha wa kadha.

Hali kadhalika, ukarabati wa uwanja ungeweza kugeuka rasilimali tosha kwa klabu, kwani baadhi ya mechi za ligi na hata za kimataifa zingeweza kutumika kwenye uwanja huo unaokadiriwa kuwa na uwezo wa kuingiza mashabiki 10,000 kama ukiwekwa majukwaa. Ndiyo, kwani ZANACO ya Zambia wanaangaika na nani zaidi ya kutumia uwanja wao wa Sunset pale Lusaka hata katika mechi za kimataifa? Kwa nini Yanga ishindwe?

Hapa ndipo ninapojiuliza kwamba ni kweli Manji aliingia Yanga kutokana na kuwa na Yanga-damu, kwa maana ya ukereketwa au alikuwa na yake?

Na katika yake, suala la ubinafsi haliwezi kuwekwa kando, kwamba pengine ana malengo ya baadaye ya kutaka kunufaika na klabu, iwe kisiasa, kimichezo, kiuchumi na njia nyingine kadha wa kadha.

Ikumbukwe kwamba, wao waliopita Yanga na klabu nyingine kubwa nchini kwa staili ya Manji, wakanufaika walivyoweza, wengine wakipenya katika makujwaa ya kisiasa na kuukwaa uheshimiwa, lakini hawakuonekana tena katika klabu zao.

Je, huko ndiko anakoelekea Manji au ana dhamira ya kweli ya kuisaidia Yanga? Kama ndivyo, kwanini asiijengee misingi imara wakati huu, na badala yake anatumia mamilioni kwa mamilioni ya shilingi kuilaza timu hotelini ilhali Yanga ina nafasi kubwa, isipokuwa yenye kuhitaji matengenezo madogo tu?

Kwa mtazamo wangu mdogo, anayoifanyia Yanga ni kama kiinimacho, haina tofauti na sherehe kubwa katikati ya msiba. Manji afahamu kwamba, Yanga inahitaji fedha zake kwa mambo mengi zaidi ya usajili huu kufuru.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments