Simba yaitafuna APR katika Kombe la Kagame baada ya kipigo cha 2-0

Wachezaji wa Simba ya Dar es Salaam wakishangilia baada ya kuifunga 2-0 timu ya APR ya Rwanda katika michuano ya Kombe la Kagame, jijini Dar es Salaam Jumanne

SIMBA, ikicheza kwa uelewano mkubwa, jana ilikata tiketi ya kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Kagame ilipoilaza APR ya Rwanda kwa mabao 2-0 na kuivua ubingwa, huku Mussa Hassan ‘Mgosi’ akirekodi bao lake la nne kwenye mashindano hayo.

Ushindi huo, uliopatikana katika dakika 20 za mwisho na ambao unaifanya timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi kukata tiketi ya kukutana na mabingwa wa Uganda, URA, umeondoa unyonge wa Simba kwa vigogo hao wa Rwanda, ambao waliilaza Simba katika fainali ya michuano hiyo ya mwaka 2004 na pia kushinda mwaka juzi wakati michuano hiyo ilipofanyika Dar es Salaam.

Awali, URA ilifanikiwa kutinga nusu fainali baada ya kuishinda Miembeni ya Zanzibar kwa mabao 2-0 katika mechi ya kwanza ya robo fainali iliyochezwa kwenye uwanja huo wa Taifa kuanzia saa 7.45.

Hata hivyo, Simba ilibidi kufanya kazi ya ziada kuweza kupata ushindi huo baada ya kipa wa APR, Aime Ndizeye kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Caleb Amwayi kutoka Kenya katika dakika ya 22 kwa kosa la kumuangusha Mgosi katika eneo la penati katika dakika ya 22.

Ikimtumia Emmanuel Gabriel kwa mara ya kwanza katika michuano hiyo, Simba ililishambulia lango la timu hiyo ya jeshi kwa muda mrefu lakini ikashindwa kuziona nyavu hadi wakati wa mapumziko.

Kuingia kwa Wanigeria, Emeh Izuchukwu na Obina Orjin kuliifanya Simba ipate mbinu za kuipenya ngome ya APR. Ushirikiano wa washambuliaji hao walioazimwa Simba na Enyimba FC ulizaa matunda katika dakika ya 79 wakati Izechukwu alipompa pasi murua Obina, ambaye alifunga kirahisi.

Dakika nane baadaye, Mgosi aliandika bao la pili baada ya kuwatoka walinzi wa APR na kuachia kiki kali iliyomshinda kipa Ndoli Claude, aliyeingia badala ya Ndizeye. Claude alionekana kupoteza muda kusubiri penati kabla ya Simba kuandika bao la kwanza.

“Tunashukuru tumeshinda kwa sababu mechi hii ilikuwa ngumu mno,” alisema kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio kabla ya kutumbukiza moja ya maneno yake ya kutamba.

“Hatuwezi kufungwa na timu ambayo imepitia dirishani wakati sisi tumepitia mlangoni. Tumewaonyesha mlango ulipo na wametoka”

Alikuwa akimaanisha kitendo cha timu hiyo ya Rwanda kusonga mbele kwa tiketi ya mshindi bora wa tatu baada ya Yanga na Miembani kuchukua nafasi za kwanza kwenye Kundi C.

Julio aliendelea kusema: “Wachezaji wangu wamecheza vizuri katika mechi zote na wamefuata maelekezo. Kipindi cha kwanza walikuwa na presha ndio maana hawakuweza kufunga, lakini walibadilika na kusahihisha makosa katika kipindi cha pili.

Kocha wa APR, Rene Feller hakutaka kuzungumza na waandishi akidai kuwa mikutano ya waandishi baada ya mechi hufanywa na makocha wakuu tu.

APR, ambayo ilifungwa mabao mawili ya haraka na Yanga, ilicheza vizuri katika kipindi cha kwanza, lakini ikakosa ujasiri wa kuingia langoni mwa Simba na ilionekana kuathiriwa na tatizo la keleleza mashabiki katika kipindi cha pili iliporuhusu mabao mawili katika muda mfupi.

Simba: Amani Simba; Antony Matangalu, Ramadhan Wasso, Juma Jabu, Kelvin Yondani, Meshack Abbel; Henry Joseph, Nicholas Nyagawa, Ulimboka Mwakingwe, Ramadhani Chombo ‘Redondo’, Adam Kingwande; Emmanuel Gabriel, Mussa Hassan ‘Mgosi’.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments