Yanga yaitungua Miembeni kwa penati Kombe la Kagame

Bonface Ambani wa Yanga akimilki mpira huku Thomas Maurice wa Miembeni pia akijaribu kuuwania katika pambano la Jumamosi mjini Dar es Salaam. Yanga ilishinda kwa bao 1-0.

*Simba yatozwa faini dola 350 kuwa kukosa nidhamu

Na Vicky Kimaro

BAO la penalti la Kigi Makassi, dakika ya 23 ya mchezo limeibeba Yanga na kuivusha hadi robo fainali dhidi ya Miembeni ya Zanzibar katika mchezo wa Kombe la Kagame uliochezwa jana kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania, jijini Dar es Salaam.

Kipa wa Miembeni, Farouk Ramadhan alimchezea madhambi Vincent Barnabas aliyekuwa amepokea pasi ya Mrisho Ngassa. Kipa Farouk alipumzishwa kipindi cha pili na kuingia Mbarouk Suleiman, ambaye aliokoa nafasi kadhaa za wazi.

Lakini, Yanga ambao walichezesha kikosi tofauti na kile kilichoanza dhidi ya APR ya Rwanda na kuwaacha nje nyota, wakiwamo kipa Juma Kaseja, Athuman Idd, ambaye hata hivyo aliingia kipindi cha pili walicheza vizuri, ilikuwa na upungufu mkubwa la kukosa umakini katika safu ya ushambuliaji na hivyo kukosa mabao mengi, hasa katika kipindi cha pili.

Kipa Mbarouk Suleiman, aliyewahi kucheza Yanga kwa upande wake alionyesha umakini mkubwa kwa kuweza kuokoa mabao ya wazi, wakati mwingine kutokana na makosa ya mabeki wake au kushindwa kufunga mabao kwa washambuliaji wa Yanga, akiwamo Ngassa na Jerry Tegete aliyeingia kipindi cha pili.

Katika hatua nyingine, Baraza la Vyama vya Soka, Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) limeitoza klabu ya Simba faini ya dola 350 (Sh402,500) kutokana na makosa kadhaa yakiwamo ya mashabiki wake kurusha chupa za maji wakati wa mechi dhidi ya BenadirTelecom ya Somalia, Alhamisi .

Makosa mengine ni kwa wachezaji wake, Ally Mustafa na Juma Jabu kuvaa jezi tofauti na zilizosajiliwa, ambao wametozwa dola 5 kila mmoja huku kipa mwingine Amani Simba akitozwa dola 15 kwa utovu wa nidhamu.

Nako katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Rayon Sports ya Rwanda ilifuzu kuingia robo fainali baada ya kuichakaza Awassa City ya Ethiopia kwa mabao 2-0 na hivyo kuungana na Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) kusonga mbele.

Hata hivyo, bingwa mtetezi, APR inasubiri hatima yake ya ama kuingia robo fainali au kuondolewa. Inaweza kufuzu kama timu bora iliyoshindwa kutoka Kundi A, ikiwania nafasi hiyo na Awassa City, kutoka Kundi B la Morogoro.

Katika mechi za leo, Simba leo itatupa karata yake ya mwisho dhidi ya Vital’O ya Burundi ambayo imeonyesha kubadilika ikilinganishwa na mchezo wa awali ambao iliadhiriwa na Benadir kwa mabao 2-1, kabla ya kuzinduka na kuwafunga Tusker ya Kenya kwa mabao 3-1.

Tusker, kwa upande wao wanakamilisha mechi za Kundi A ambalo bado lipo wazi kutokana na kila timu kuwa na pointi tatu itakapocheza na Benadir, saa 8 mchana, ikifuatiwa na Simba dhidi ya Vital’O saa 10 jioni.

Vikosi katika mchezo wa jana vilikuwa:

Yanga: Ivo Mapunda, Nurdin Bakari, Shadrack Nsajigwa, Wisdom Ndhlovu, George Owino, Godfrey Bonny, Shamte Ally, Mrisho Ngassa, Boniface Ambani, Vincent Barnabas

Miembeni:

Farouk Ramadhan, Mwinyi Ally Deo, Amour Omar, Lulanga Mapunda,Samson Mwamanda,Adam Juma,Amri Kiemba, Sabri Ramadhan, Thomas Maurice, Maulid Ibrahim Kapenta

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments