Hongera vijana wa U-17

MWISHONI mwa wiki, timu ya vijana ya U-17 ya Tanzania iliyochaguliwa katika michuano ya Copa Coca Cola yaliyomalizika hivi karibuni, imetwaa ubingwa wa michuano hiyo ngazi ya kimataifa iliyofanyika Brazil baada ya kuifunga Chile mabao 2-1 katika mechi ya fainali.

Ushindi wa timu hiyo umehitimisha michezo yake bila kupoteza mchezo hata mmoja, ilianza kwa kuilaza Peru mabao 5-0, ikatoka suluhu na Chile kabla ya kuilaza Argentina mabao 2-0. Iliishinda Argentina 2-0 katika robo fainali na kuilaza Paraguay 3-1 kwenye nusu fainali.

Hiyo pekee inaonyesha kwamba vijana waliochaguliwa, ni kweli wenye vipaji ambavyo hawatakiwi hata mara moja kuvipoteza. Shirikisho la Soka Tanzania, TFF na wadau mbalimbali wa soka wanatakiwa kuviendeleza vipaji vya vijana hawa kwa kuwa tayari wameshaonyesha wanaweza.

Kutwaa ubingwa wa bonanza hilo la kimataifa kwa Academy mbalimbali za soka duniani, ni kielelezo kwamba vijana wa Tanzania soka wanaiweza, na kwamba wanastahili kuendelezwa kwa kupatiwa vifaa, walimu pamoja na kupata elimu ya soka, ndani na nje ya uwanja.

Wakati michuano hii inaanza mwaka jana, kila mmoja alihamasika kuona kuwa sasa Tanzania inaanza kuangalia eneo la vijana, na mataifa mbalimbali yamekuwa yakianza na umri kai ya miaka 14 hadi 20.

Sasa kwa kuanzishwa kwa mashindano ya Copa Coca Cola ni wazi kuwa Tanzania imepania kikwelikweli kuendeleza soka kwa kuanzia na vijana. Ikimbukwe kuwa hakuna soka inayoanza kwa kuchukuliwa wachezaji wa vijiweni. Imekuwa ni kawaida kwa timu kubwa kwenda kwenye mashindano ya nchangani ambako huko huanza kusaka wachezaji wanaong’ara na kuwaleta katika Ligi Kuu. Pamoja na kwamba wachezaji walikuwa na vipaji, lakini si hivyo.

Wachezaji wanatakiwa kuwa na maandalizi, ndiyo maana mara kadhaa wamekuwa wakikwama kucheza soka nje kwa kuwa hawakutokea kwenye academy yoyote inayowatengeneza. Mchezaji anatakiwa kuandaliwa, kucheza soka ndani na nje ya uwanja.

Itakumbukwa katika miaka ya nyuma, wapo wachezaji waliobahatika kupata timu, lakini walipoulizwa historia ya Academy aliyowahi kuishi, hakuna.

Hapo ukawa mwisho wa mawasiliano. Sasa wachezaji kama hawa, wanatakiwa kuendelezwa kwa nguvu zote. Tayari TFF imeshasema kuwa wachezaji hao wa Brazil watapelekwa katika shule ya soka ikiwa ni motiosha ya shirikisho hilo kwa vijaa kwa kuwa wamefanya mambo makubwa wakiwa Brazil.

Katibu Mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela alisema kuwa vijana hao wataunganishwa na wengine 25 walioko kwenye shule ya TFF na watakuwa wakisoma na kucheza soka ya mafunzo. Tunaupongeza uamuzi huo wa TFF kwamba utakuwa changamoto kwa vijana kwa mwaka utakaofuata.

Kwa kuwa utaratibu wa kusomesha umeanza, TFF iendelee kusaka wadhamini kwa ajili ya kujenga shule zaidi za soka kwa ajili ya watoto hao ambao hupatikana kila mwaka. Vijana hao ambao wanawasili leo kutoka Rio de Jeneiro, Brazil tunawakaribisha nyumbani lakini wakumbuke kuwa huo ni mwanzo wao wa soka na si kubweteka na kujisahau. Wanatakiwa kujifunza zaidi na zaidi.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments