Somalia yashangaza kwa kuifunga Burundi michezo ya Kagame

HUKU kocha wa APR, Rene Feller akishindwa kuamini timu yake kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na Yanga na wachezaji wake kuwahofu wawakilishi hao Tanzzania Bara kwa uwezo mkubwa wa kufika fainali, mshangao wa kwanza wa michuano hiyo umetokea jana baada ya Benadir ya Somalia kuilaza Vital’O ya Burundi mabao 2-1.

Juzi, baada ya mechi hiyo ya Kundi C, Mbuyu Twite, kiungo aliyefunga mabao mawili ya APR kwa mikwaju ya adhabu, alisema kuwa Yanga imeonyesha soka safi na kwamba hadi sasa ndiyo timu bora kwa Tanzania baada ya kuiona Simba ikilambwa mabao 3-2 na Tusker katika mechi ya ufunguzi.

Jana, nahodha wao, Ntaganda Elias hakuficha kilicho moyoni mwake alipochambua mchezo huo katika mahojiano na Mwananchi.

Nahodha huyo alidai kuwa walikuwa wana uhakika wa kushinda mchezo huo baada ya kucheza vizuri dhidi ya Yanga, lakini akaeleza kushangazwa na jinsi mchezo ulivyomalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Lakini baadaye akasema: Yanga inacheza soka la kiwango cha juu kati ya timu zote ambazo nimewahi kuziona tangu kuanza mashindano hayo.

” Wanajitahidi kucheza kwani hata sisi hatukutegemea kupata ushindani wa namna hiyo. Nawasifu sana mabeki wao kwa kuwa wako makini mno. Wana ukuta imara sana hilo nawapa sifa.

Kutokana na Yanga kucheza soka la kueleweka, nina imani kuwa watafika fainali na inaweza kuwa ni kati ya APR na Yanga.

“Fainali lazima tukutane tena. Labda wao watereze, lakini sisi tuna uhakika wa kufika fainali, na wao kama wataendelea hivyo hivyo na moto wao basi tutakutana tena fainali hilo halina ubishi.”

APR walicheza kwa pasi fupifupi wakijongea langoni mwa Yanga, ambao badala yake kila walipopokonya mipira walipiga pasi ndefu kwa washambuliaji wao, Boniface Ambani na Mrisho Ngassa, walioisumbua sana ngome ya Wanyarwanda.

Moja ya mipira hiyo mirefu ndiyo iliyozaa bao la kwanza wakati Ambani alipoubetulia kwa kichwa mpira juu uliomkuta beki mmoja wa APR katika nafasi mbaya kabla ya Jerry Tegete kuuzuia na kumfikia Ngassa aliyefunga kirahisi.

Katika mfululizo wa michuano ya Kagame, Benadir ya Somalia imeshangaza wengi kwa kuilaza Vital’O ya Burundi kwa mabao 2-1 katika mchezo wa Kundi A.

Vital’O ambao waliwasili Dar es Salaam jana kwa basi wakitokea Bujumbura, walionekana wachovu na kuwaacha Wasomali hao ambao ni nadra kutamba katika michuano kutamba na kupachika mabao hayo, yote katika kipindi cha pili.

Hata hivyo, mchezo huo ulishuhudia kadi ya kwanza nyekundu wa michuano hiyo kutoka kwa mwamuzi Waziri Sheha wa Zanzibar ambazo alimpa Yassin Ali wa Benadir baada ya kumchezea vibaya Akakimana Ndizeye wa Burundi.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments