Simba yaanza vibaya Kombe la Kagame yapigwa 3-2 na Tusker Kenya

Mchezaji kiungo wa Simba ya Tanzania, Henry Joseph akiwatoka wachezaji wa Tusker ya Kenya, katika mchezo wa fungua dimba wa Kombe la Kagame kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam jana. Simba ililala 3-2.

SIMBA imeanza vibaya michuano ya Kombe la Kagame baada ya kufungwa na Tusker ya Kenya mabao 3-2 katika mchezo wa ufunguzi ambao pia imeifanya michuano hiyo ianze kwa karamu ya mabao.

Mchezo huo hata hivyo, ulionyesha kasoro kadhaa hasa katika safu ya ulinzi ya timu hizo mbili.

Hadi mapumziko, ngome za timu hizo zilikuwa zimeruhusu mabao manne na kufanya matokeo kuwa mabao 2-2.

Tusker ya Kenya ilianza kuhesabu bao la kwanza la michuano hiyo, dakika ya tisa kupitia kwa Humphrey Okoth baada ya beki Kelvin Yondani wa Simba kuokoa kizembe na mpira kumkuta Daniel Matego aliyempa pasi mfungaji.

Dakika ya 22, Simba waligongeana vizuri kati ya mabeki Salum Kanoni na Yondani kutoa krosi kwa Ulimboka Mwakingwe aliyemsogezeaMnigeria Emeh Izichukwu, ambaye hakung’ara aliyemrudishia Mwakingwe akaachia mkwaju uliomshinda kipa Joseph Ruto wa Tusker.

Adam Kingwande, aliweza kujiandika katika orodha ya wafungaji wa michuano hiyo baada ya kupachika bao la pili kwa timu yake, dakika ya 29 kwa mkwaju mkali baada ya kupokea pasi ya Kanoni.

Lakini, furaha ya Wekundu wa Msimbazi ilidumu kwa muda mfupi baada ya Tusker kupata bao la kusawazisha, dakika ya 45 kupitia kwa Simon Mburu kutokana na uzembe wa mabeki.

Kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza, Tusker walizifumania nyavu za Simba dakika ya 51 la John Kio, ikiwa ni kutokana na makosa ya mabeki na kipa Ally Mustapha.

Kocha wa Simba, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ alifanya mabadiliko kipindi cha pili kwa kuwaingiza Aziz , Haruna Moshi , Jabir, Mnigeria Obina Orji, lakini hayakuisaidia Simba.

Julio, alisema kipigo hicho ni matokeo ya uzembe wa mabeki wake waliojiamini kupita kiasi, lakini aliahidi kujipanga vizuri kwa ushindi katika mechi zinazofuata.

Kocha wa Tusker, ‘Jacob Ghost’ Mulee alisema kuwa walicheza kwa kusaka sare kutokana na uchoyo wa safari, lakini ushindi umempa faraja na kuongeza kuwa Simba na Tusker watasonga mbele kutoka Kundi A.

Kikosi cha Simba jana kilikuwa:

Ally Mustapha, Salum Kanoni, Ramazan Wasso, Kelvin Yondani, Henry Joseph, Mohammed Banka, Mussa Hassan Mgosi/Haruna, Ramadhan Chombo/Orji Obinna, Adam Kingwande/Jabir Aziz, Emeh Izichukwu, Ulimboka Mwakingwe

xxxxxxxxxxxxx

Yanga yabeba matumaini

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya jana kuishuhudia Simba ikilizwa mabao 3-2 na Tusker ya Kenya, leo ni zamu ya Yanga kuwakabili mabingwa watetezi, APR ya Rwanda katika mchezo wa Kundi C utakaofanyika kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa.

Yanga, ikiwa na silaha zake zilizoandaliwa mahsusi kwa michuano hiyo na ile ya kimataifa itaingia kwenye uwanja kwa tahadhari kubwa.

Yanga, ambayo katika michezo ya kujinoa iliilaza Express ya Uganda kwa bao 1-0 na pia kuizima Mbagala Market kwa mabao 2-0, inabeba jukumu la kuanza vizuri ili kurejea imani ya mashabiki wake na Watanzania.

Lakini, Yanga inatarajia upinzani mkali kutoka kwa vijana wa APR, askari wanaodhaminiwa na Rais wa Rwanda, Paul Kagame.

APR, ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hii waliwasili nchini wakidai kuwa wametumwa na Rais Kagame warejee Kigali na kombe hilo.

Huenda kazi kubwa kwa Yanga leo ikawa ya kumkabili mchezaji wanayemjua , mwenye uwezo wa kuzunguka uwanja mzima, Mkenya Moses Odhiambo aliyekuwa Simba.

Huenda Yanga leo ikapangwa:

Juma Kaseja, Shadrack Nsajigwa, Nurdin Bakari/Mbuna, Wisdom Ndhlovu, George Owino, Godfrey Bonny, Mrisho Ngassa, Athuman Idd, Laurent Kabanda, Ben Mwalala na Boniface Ambani.

xxxxxxxxxx

Viingilio vyakwaza mashabiki

Na Mwandishi Wetu

IDADI ya mashabiki waliojitokeza kuona ufunguzi na hatimaye mechi kati ya Simba na Tusker ilikuwa ndogo kinyume na matarajio ya wengi.

Licha ya kiingilio cha juu kuwa Sh25,000 na kile cha chini kuwa Sh5,000, lakini, kinyume na wengi, si mashabiki wengi waliofurika katika uwanja huo.

Viingilio hivyo, vilidaiwa kuwa vikubwa kwa walio wengi wenye uwezo, kiasi cha kulishauri Baraza la Vyama vya Soka, Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wenyeji kuvipunguza.

Walidai kuwa ingekuwa bora viingilio hivyo viwe vya chini ili kuwawezesha mashabiki wengi zaidi kuingia na kuzishangilia timu zao, Simba, Yanga na Miembeni ya Zanzibar.

Baadhi yao walisikika wakidai kuwa huenda hata mechi ya leo kati ya Yanga na APR nayo ikapungukiwa na mashabiki, endapo viingilio vitaendelea kuwa vikubwa.

Ukiachilia mbali suala la viingilio, hakukuwa na matukio makubwa, zaidi ya mashabiki kupanguliwa kutoka majukwaa ya Sh3,000 na kushushwa yale ya Sh 5,000.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments