FIFA yambwaga Aden Rage kurejea Shirikisho la Soka Tanzania

SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (Fifa), limetupilia mbali barua ya rufani ya makamu wa zamani wa pili wa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ismail Rage aliyetaka kurudishwa katika nafasi yake.

Rage alipoteza nafasi hiyo baada ya kuhukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela kwa tuhuma za wizi wa fedha za kilichokuwa Chama cha Soka Tanzania, FAT.

Awali, Kamati ya Nidhamu ya TFF iliyoketi jijini Dar es Salaam Machi 26 ilitoa tamko la kurudishwa kwa Rage katika nafasi yake ambayo kwa wakati huo ilikuwa ikishikiliwa na Jamal Bayser, lakini hata hivyo uongozi wa shirikisho hilo ulisema utalifikisha suala hilo kwa Kamati ya Utendaji ili lipate mwongozo .

Kikao hicho kilipokutana kilikataa kumrejesha Rage kwa kile kilichoelezwa kuwa tayari alikwishapoteza sifa kwa kuwa alikosa vikao vitatu muhimu vya shirikisho hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Fredrick Mwakalebela alisema kuwa Juni 24, shirikisho lake lilipokea barua kutoka Fifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wake,, Jerome Valcke likitoa msimamo wa kuyakataa malalamiko ya Rage kuhusu kurejeshwa madarakani.

Fifa imeeleza kuwa nafasi hiyo iendelee kushikiliwa na mjumbe wa kamati ya utendaji ambaye pia ni mwakilishi wa klabu.

Mwakalebela alisema kuwa barua hiyo ya Fifa ni majibu ya barua ya Rage aliyoituma kwa shirikikisho hilo Mei 13 mwaka huu akilalamika kutorejeshwa katika nafasi yake ya makamu wa pili wa TFF.

Mwakalebela alisema baada ya kupokea barua ya Rage, Fifa iliandika barua TFF ikitaarifu juu ya malalamiko hayo na kutaka ufafanuzi ambapo wao walifanya hivyo kwa kuelezea sababu zilizokwamisha suala hilo.

Alisema kuwa Katika maelezo ya kwenda Fifa, shirikisho hilo lilieleza kushindwa kutekeleza maagizo ya kamati ya nidhamu kwa vile katiba ya sasa ya TFF ilianza kufanya kazi Januari 15, 2006 na si siku ilipogongwa muhuri na Msajili wa Vyama na Klabu za Michezo Mei 2, 2006.

Hivyo, hata kama katiba ya sasa ingeanza kufanya kazi miezi 12 baadaye isingewezekana kwa Rage kurudi katika nafasi hiyo kwavile alikuwa hajasafishwa hadi Machi 19, 2008.

Alisema kuwa baada ya Fifa kuridhishwa na maelezo ya barua ya TFF , Juni 24 iliandika barua juu ya msimamo wake juu ya suala la Rage.

Aliongeza kuwa pamoja na Fifa kutoa msimamo huo, lakini pia limemshauri Rage kusubiri uchaguzi mkuu ujao wa TFF ambao unatarajia kufanyika Desemba mwaka huu ili aweze kugombea nafasi kama angependa.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments