TFF sasa inatupeleka pabaya!

KWA kitendo cha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) cha kumshupalia beki mahiri wa Taifa Stars, Nadir Haroub `Cannavaro’ airudishe jeshi ya Taifa Stars aliyompaia Samuel Eto’o Fils, nathubutu kusema shirikisho hili linatupeleka pabaya.

Bila aibu, viongozi wa TFF wanadiriki kuuambia umma wa Watanzania kwamba, lazima Nadir airudishe jezi au awe tayari kukatwa sh 20,000 za Tanzania kufikia jezi hiyo.

Nashukuru kwamba, kabla ya mshangao wao haujafika mbali, wadau wa Zanzibar wamechangishana na kupata fedha sh 110,000 kumlipia Nadir.

Hali kadhalika, wadhamini wakuu wa Taifa Stars, Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) wanaotoa kila mwaka kitita cha sh bilioni moja, nao wamekerwa, wamejitolea kulipa sh 20,000 anayodaiwa beki huyo aliyeifanyia nchi mambo makubwa, kiasi cha Eto’o kumfuata beki huyo wa Yanga na kumsihi ampatie jezi yake ya Taifa Stars mara baada ya mchezo wa marudiano huko Yaounde, Cameroon.

Katika mchezo huo wa kampeni za awali za kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010, Cameroon ilishinda kwa mbinde 2-1, huku ikibanwa mbavu katika mchezo wa kwanza jijini Dar es Salaam kwa timu hizo kushindwa kufungana.

Eto’o, Mwanasoka Bora wa Afrika mara tatu aliyewahi pia kushika nafasi ya tatu kwa ubora duniani, alikiri kwamba, pamoja na kujituma kwa Stars, Nadir aliiokoa kutokana na kucheza soka halisi ya kimataifa na kumnyima pumzi nyota huyo anayeichezea Barcelona ya Hispania.

Kwa hakika, mpenda michezo yeyote angekiona kitendo cha Eto’o cha `kumvulia kofia’ Nadir na hata kuomba ukumbusho wa nyota huyo mwenye asili ya Zanzibar, kuwa cha kishujaa kwa nyota wa Kitanzania na sifa kwa nchi pia.

Mchezaji kama Eto’o kuikumbatia jezi ya Tanzania, halikuwa jambo dogo hata kidogo.

Lakini kwa mshangao wa wengi, TFF ambayo kwa sasa haitumii hata senti moja kuiandaa Stars, zaidi ya kupokea misaada kutoka SBL, Benki ya NMB na wadau wengine, imekuja juu kuidai jezi ya sh 20,000.

Itakumbukwa kwamba, inadai jezi hiyo siku chache baada ya kuvuna zaidi ya sh milioni 500 katika mchezo na Stars, lakini ikijua haijaingia gharama za kutisha kuiandaa timu, ikiwanyonya wachezaji kwa kuwapoza sh milioni moja moja tu.

Inashangaza kwa TFF kukosa shukrani kwa mashujaa wake wanaopigana kufa au kupona kuiletea sifa nchi. Na kweli, kwa kuwabana Cameroon katika mchezo wa kwanza, hadhi ya Taifa Stars na Tanzania kwa ujumla ilipaa ajabu.

Hivi TFF inataka kutuambia nini, kwamba fedha zote za wafadhili zinashindwa kununua jezi?

Au imeamua kuishi kwa ujima wa kuwa na jezi staili ya `Kauka Nikuvae?’

Mbona jezi hizi zinazotumiwa na Stars si za kuinyima usingizi TFF kiasi hiki? Mbona hazina ubora unaotajwa kulinganisha na jezi za nchi nyingine?

Tena katika hili TFF inabidi izinduke na kuangalia ubora wa jezi, na ikibidi ianze kuandika majina ya wachezaji kwenye jezi zao. Mbona hata klabu zetu zinamudu kufanya hivyo?

Tunadhani wakati umefika wa TFF kuangalia mambo makubwa yenye mwelekeo wa kuinua soka yetu, badala ya kuhangaika ni mambo kama haya ya 20,000, tena mpaka kwenye vyombo vya habari.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga na wasaidizi wake bila shaka wanapaswa kukuna vichwa na kuangalia ni jinsi gani wanaweza kuzidi kuiamsha soka ya Tanzania iliyozirai tangu miaka ya 1980.

Kwa wafuatiliaji wazuri wa soka la Tanzania, wanafahamu fika kuwa tangu nchi hii ipate Uhuru wake mwaka 1961, hatujawahi kuwa na mafanikio yeyote zaidi ya angalau kushiriki mara moja fainali za Mataifa ya Ulaya za mwaka 1980.

Baada ya hapo timu yetu ya taifa, Taifa Stars, haijakuwa na lolote la maana na katika klabu, ni mara mbili tatu tu ndiyo tuliweza kujitutumia lakini si kwa kutamba kwa ubingwa katika michuano ya barani Afrika.

Tatizo si wachezaji, bali watu wanaopewa dhamana ya kuongoza soka, ni umbumbumbu wa uongozi wa kisoka ndiyo unaotusumbua.
Ndiyo maana tunaona na kusikia vitu visivyopaswa kuzungumzwa katika zama hizi, kama hili la kudai jezi.

Inashangaza kabisa. Hivi viongozi wa TFF ni viongozi wa soka kweli? Ni wanamichezo halisi kweli?

Kuna kosa gani kwa Cannavaro kumpa jezi Eto’o ambaye pamoja na umahiri wake katika ulimwengu wa soka alifikia hatua ya kukiri kuwa Cannavaro ni kiboko hadi kumpa jezi yake kama ukumbusho?

Kwetu tunadhani kitendo cha Eto’o kukiri kuwa Cannavaro ni kiboko, kilipaswa kuchukuliwa kama kichocheo kwa beki wetu huyo apewe moyo zaidi ili ongoze jitihada.

Na alichofanya Cannavaro ni kitendo cha uanamichezo kabisa, leo anaadhibiwa kwa kosa lipi, au ni umbumbumbu wa watu wa TFF?

Kama TFF inang’ang’ania jezi ya Cannavaro, kitu ambacho katika ulimwengu wa soka ni kidogo sana, inaanza sasa kutupa shaka ya mambo mengi.

Maana wana saikolojia husema, aliye mwangalifu na muadilifu katika mambo madogo, huwa hivyo hata kwa makubwa, kwani makubwa hujengwa na madogo. Kinyume cha hivyo ni dalili ya kuwepo matatizo.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments