Tenga amshushua Kaijage kuhusu jezi

Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Leodger Tenga jana ameyafuta maneno ya Afisa habari wa Shirikisho hilo, Florian Kaijage ya kumdai jezi ya timu ya taifa, Taifa Stars, Nadir Haroub `Cannavaro`, ambaye alibadilishana jezi hiyo na mchezaji wa kimataifa wa Cameroon, Samuel Eto`o.

Haroub, alibadilishana jezi na Eto`o mara baada ya mchezo wao wa marudiano wa kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia na zile za mataifa ya Afrika uliochezwa, nchini Cameroon.

Mara baada ya mchezo huo Eto’o alimfuata Haroub na kumkumbatia kisha alimuomba wabadilishane jezi ikiwa ni ishara ya upendo kwenye mchezo wa soka.

Hata hivyo, kitendo hicho kilionekana kama dhambi kwa baadhi ya viongozi wa TFF, ambapo muda mfupi mara baada ya timu kurejea nchini Kaijage alitangaza kukatwa posho ya sh. 40,000 ili kulipia jezi hiyo.

Kauli ya Tenga inaashiria kuwa Kaijage, ambaye ni msemaji wa shirikisho hilo, aliamua kudai jezi hiyo bila ya baraka za viongozi wa juu wa TFF.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Tenga alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Haroub ni cha kishujaa, kilichojaa uungwana, ambapo anastahili kupongezwa kwa hatua yake hiyo ya kuitangaza nchi kimataifa.

Tenga, alisema kuwa jezi ya timu ya Taifa ni sawa na bendera ya taifa, hivyo halikuwa tatizo kwa Haroub kubadilishana jezi na Etoo, ambapo kitendo hicho ni cha kawaida kufanyika duniani kwani kinachangia kuitangaza nchi.

“Nimeshangazwa na hatua iliyochukuliwa ya kumdai Haroub jezi, huyu kijana amefanya kitendo cha kishujaa na anastahili pongezi kwa kuitangaza nchi kimataifa, si jambo jema kwa shujaa, kazi aliyoifanya ni ya kibalozi, naagiza posho ya mchezaji huyu na mwingine yeyote aliyefanya hivyo asikatwe chochote,“alisema Tenga.

Tenga pia aliagiza kila mchezaji wa Stars, atakuwa anaondoka na jezi atakayoitumia kwenye kila mchezo hata kama atakuwa ni mchezaji wa akiba.

  • SOURCE: Nipashe

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments