Serengeti Boys kunolewa na Kocha Perreira BrazilTIMU ya soka ya vijana walio chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys, itaondoka nchini Juni 5 kuelekea Brazil , ambako itakuwa chini ya kocha aliyeiongoza Brazil kutwaa Kombe la Dunia mwaka 1994, Carlos Alberto Perreira.

Mratibu wa mashindano ya Copa Coca-Cola, George Rwehimbiza alisema timu hiyo itafikia kwenye kituo cha michezo cha Brazil Football Academy, na itaondoka na viongozi wanne akiwemo kocha mkuu wa timu ya vijana, Marcus Tinocco.

“Timu itaondoka Juni 5 kuelekea Brazil itakaa huko kwa muda wa wiki moja,” alisema Rwehimbiza. “Timu itafikia kwenye kituo hicho kilicho chini ya Carlos Alberto Perreira.”

Perreira aliiongoza Afrika Kusini kwenye fainali za Mataifa ya Afrika mapema mwaka huu, lakini akajiondoa kwenye kazi hiyo hivi karibuni, akieleza kuwa mkewe alikuwa ni mgonjwa.

Vijana watakaokuwa kwenye safari hiyo watapatikana kutoka katika mashindano ya Copa Coca-Cola yanayoeelekea ukingoni jijini Dar es salaam baada ya kuendeshwa kwa takriban wiki mbili.

Mashindano hayo yanashirikisha timu za kombaini za mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani, zikiwemo wilaya za Ilaya, Kinondoni na Temeke zilizopewa hadhi ya mkoa.

Vijana wengi walioteuliwa kwa ubora katika mashindano ya kwanza yaliyofanyika jijini Dar es salaam kwa sasa wanasomeshwa na Shirikisho la Soka (TFF) kwenye shule ya sekondari ya Jitegemee, ambako huhudhuria vipindi vya masomo ya kawaida na yale ya soka.

Wakati huohuo, kocha Tinoco amesema kuwa hatapata kazi kubwa ya kuwanoa vijana 17 watakaopatikana katika michuano ya Copa Coca-Cola, anaripoti Sosthenes Nyoni.

Akizungumza baada ya mechi baina ya timu ya mkoa wa Kigoma na Kusini Pemba, Tinocco alisema kuwa hilo linatokana na wachezaji wengi kuonekana kuwa wamefundishika.

Alisema kuwa tofauti na mwaka jana mashindano ya mwaka huu yameonyesha baadhi walimu wa timu shiriki kuwa wana uwezo mkubwa wa kufundisha soka na ndio maana baadhi ya timu zinacheza soka lenye mpangilio.

Imeeandikwa na MWANANCHI

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments