ZFA yadaiwa kuibeba Miembeni

Chama cha soka cha Zanzibar, ZFA, kimeshutumiwa kuwa kimekuwa kikipangua mara kwa mara ratiba ya ligi kuu ya Zanzibar ili kuiweka timu ya Miembeni katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wake.

Aidha, ZFA imelaumiwa pia kuwa na njama za kuipendelea Malindi kwa kumpanga mwamuzi mmoja aliyetajwa kwa jina la Kisaka kuchezesha mechi zote za timu hiyo.

Kocha mkuu wa timu ya Mundu na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Zanzibar Hemed Morocco aliliambia Lete RAHA kwa njia ya simu katikati ya wiki kuwa kwa sasa hakuna haki katika soka visiwani kutokana na ZFA kuzikumbatia baadhi ya timu ili zitwae ubingwa, na nyingine zibaki katika ligi hiyo.

“Tunaomba mtusaidie hawa wenzetu hakuna wanachofanya zaidi ya malumbano yasiyokuwa na msingi, sasa hakuna soka kabisa Zanzibar, yaani ungeona mechi yetu na Malindi kama kweli ni mpenzi wa soka hutapenda kabisa kuja tena uwanjani kutazama, waamuzi wanafanya madudu ya wazi wakipendelea timu hizo,“ alisema Morocco.

Mundu imeongoza ligi kuu kwa muda mrefu na pamoja na Miembeni ndiyo zenye uwezekano mkubwa wa kutwaa ubingwa.

Alisema Malindi imecheza mechi moja pungufu baada ya mchezo dhidi ya KMKM kuahirishwa na haijulikani utachezwa lini.

Hatahivyo, alisema pamoja na hujuma zote wanazofanyiwa bado wana uhakika wa kuwavua ubingwa Miembeni kutokana na ubora wa timu yake ambao hautegemei kubebwa na mwamuzi.

Malindi iliyokuwa kwenye janga la kushuka daraja imechupa kutoka nafasi ya 10 hadi ya saba baada ya kushinda mechi sita na kutoka sare mara tano katika michezo 17. Timu nne, kati ya 12, zitashuka daraja kwa mujibu wa kanuni.

  • SOURCE: Lete Raha

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments