Ndoto ya Taifa Stars yayeyuka

NI dhahiri kwamba, ndoto yetu ya kucheza ama fainali za Kombe la Dunia au Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2010, sasa zimefikia ukingoni.

Timu yetu ya soka ya taifa `Taifa Stars’, ingawa mebakiwa na mechi mbili mkononi dhidi ya Cape Verde na Mauritius kukamilisha awamu ya kwanza ya mchujo wa fainali hizo, hatuna matumaini tena.

Cameroon wameshatangulia wakifuatiwa na Cape Verde wanaotofautiana kwa pointi moja tu katika Kundi la Kwanza, huku Cameron ikiwa kileleni kwa pointi kumi. Stars iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili na Mauritius inashika mkia. Ina pointi moja.

Kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na FIFA, Shirikisho la Soka la Kimataifa na lile la Afrika (CAF), mshindi wa kila kundi kati ya 12 ataingia moja kwa moja katika hatua ya pili ya michuano kuungana na timu nane bora kutoka katika makundi 12.

Hii ina maana kwamba, ngwe inayofuata itakuwa na timu 20 zitakazogawanywa katika makundi matano, lenye timu nne kila moja. Huko, mshindi wa kila kundi atafuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na timu tatu za juu kutoka kila kundi zitacheza fainali za Afrika huko Angola.

Ndiyo maana tunasema, kwa kuwa tumekosa nafasi ya pili katika mchujo wa awali, michuano yote, ya Kombe la Dunia na ile ya Afrika kwa mwaka 2010 inabaki kuwa historia, labda tubahatishe mwaka 2012 katika fainali za 28 zitakazoandaliwa kwa ushirikiano baina ya Gabon na Equatorial.

Ni kubahatisha kwa sababu tangu mwaka 1980 nchini Nigeria, hatujabahatika kufuzu tena, licha ya mara kadhaa kukaribia, kumbukumbu za karibu zikitupeleka katika fainali za mwaka huu huko Ghana.

Wengi waliamini chini ya Mbrazil Marcio Maximo, mambo yangekuwa shwari. Tuliteleza, tukazidiwa kete na Senegal na dakika za mwisho na Msumbiji.

Ikaingia homa ya 2010, kila mmoja akiamini kama si Kombe la Dunia, basi michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika itakuwa saizi yetu, lakini hadithi imejirudia, kwamba tutaendelea kuhaingaika na Chalenji na pengine mechi za kirafiki, basi.

Michezo yetu iliyobaki ni ya kujenga timu ya miaka ijayo, kama nyota wetu watafundishika.

Inasikitisha sana kuona juhudi kubwa zinafanyika, lakini maosa madogo madogo yanaigharimu timu.

Hebu fikiria, Maximo pamoja na kuunda kikosi imara kinachogeuka gumzo, hawezi kusimama mbele ya watu na kuringia safu kali ya ushambuliaji au ubora wa makipa wake, hata ikibidi huyo anayemtegemea kwa sasa, Ivo Mapunda.

Nafasi hizo zina matatizo, lakini kubwa linaloonekana kuiangusha Stars hii inayoonekana kujengeka upya na kucheza soka la kisasa, ni ubutu wa safu ya ushambuliaji.

Kimekuwa kilio kuanzia katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara hata kwenye timu ya taifa, ni matatizo matupu.

Lakini tukubali kwamba, hakuna timu inayoweza kushinda bila kupata magoli. Ushindi unatokana na magoli. Mpira mabao, kama huna jeuri ya kufunga, ni wazi siku zote matokeo ya uwanjani hayawezi kuwa mazuri.

Yaelekea kama ilivyo kwa makocha wazalendo, hata Maximo anapasua kichwa, baada ya kufanya kazi kwa miaka miwili lakini akikosa suluhu katika safu ya ushambuliaji. Amebadilisha sana washambuliaji, kuanzia akina Mwaikimba (Gaudence), Machupa (Athuman), Joseph Kaniki, Gulla Joshua, Emmanuel Gabriel, Yona Ndabila na hata Haruna Moshi `Boban’, lakini ni wachache wanaoonyesha uchu kama dalili zinayoanza kuonekana kwa Danny Mrwanda aliyeongezewa makali ya soka na klabu yake ya Al Tadhamon ya Kuwait.

Tatizo la ubutu wa washambuliaji hapa nchini limeota mizizi kuanzia ngazi za klabu. Makocha wote kwenye kilabu vya Ligi Kuu wanalalamikia washambuliaji wao kukosa mabao.

Maximo amejaribu karibu washambuliaji wote wanaowika katika Ligi Kuu Tanzania Bara na Visiwani na hata wale waliokuwa wanapigiwa debe na washabiki wa soka hapa nchini, lakini hakuna aliyeweza kulimaliza tatizo hili.

Hakuna tena washambuliaji wenye uchu na umahiri wa kupachika mabao kama ilivyokuwa kwa akina Peter Tino, Kitwana Manara, Zamoyoni Mogela, Kitwana Suleiman, Edward Chumila, Edgar Fongo, Abeid Mziba, Bita John, Fumo Felician, Mohammed Hussein `Mmachinga’. Orodha ni ndefu. Yatosha kusema na wengine.

Uthibitisho wa ukame wa mabao kwa nyota wazalendo unaweza kuthibitika kutokana na idadi ndogo ya mabao inayopatikana katika mechi za ligi na hata za kimataifa kwa upande wa klabu.

Tuchukulie mfano mdogo tu wa Ligi Kuu yetu; Mfungaji Bora ni Mike Katende wa Kagera Sugar, huyu si Mtanzania ni Mganda aliyefunga mabao 11 katika mechi 26 za Ligi Kuu.

Nafasi ya pili katika ufungaji bora iling’ang’aniwa na wachezaji wanne,’ Mourice Sunguti, yeye ni Mkenya anayecheza Yanga, Osward Morris na Yona Ndabila wa Prisons ya Mbeya na Philip Alando wa Toto Africa ya Mwanza wao ni Watanzania. Walifunga magoli tisa kila mmoja.

Nyuma yao kwenye nafasi ya tatu alikuwepo Moses Odhiambo, Mkenya aliyeichezea Simba na kufunga magoli manane. Kwa sasa ametimkia Rwanda kuichezea APR ya huko.

Tujiulize, ingawa si mabao mengi yaliyofungwa kiasi cha mchezaji kuringia tuzo ya ufungaji bora, kwa nini hata hayo mabao machache yametawaliwa na wageni? Kwa Yanga, Sunguti ndiye aliyeongoza, kule Simba ni Odhiambo, Katende ni Kagera.

Tufanyeje? Yaelekea ndiyo maswali wanayojiuliza wadau wengi wa soka nchini. Lakini yafaa kuamini kwamba, kwa juhudi za pamoja inawezekana. Kinachotakiwa ni kumpa muda zaidi Maximo na wasaidizi wake kuangalia vipaji vipya kama alivyoweza kubaini ubora wa Jerry Tegete na Amos Kigi ambao bado wanapevuka, ingawa mara moja moja wanajaribu.

Si Maximo pekee, hata kocha wa vijana `Serengeti Boys’, Marcos Tinocco naye anapaswa kuzinduka na kuyaangalia vyema majukumu yake, kwani haonekani kusaka vipaji, licha ya kuwa nchini kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Tinocco anaweza kuwa mhimili mzuri wa kufukuza jinamzi la ubutu wa washambuliaji wetu, lakini kama atasaka vipaji na kuviendeleza, hivyo kumrahisishia kazi Maximo katika kuwaka raha Watanzania.

Haitoshi tu kucheza soka kwa staili ya chenga twawala, lakini mwisho wa siku tukigeuzwa kapu la pointi.

Kwa juhudi za pamoja, yawezekana milango ya miujiza kwa Stars ikafunguka, lakini lazima kuwe na mikakati thabiti ili `Ndege ya Mwaka 2012 Isituache’.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments