Mashujaa wafa kiume cameroon

Na Angetile Osiah, Cameroon

TAIFA Stars wakicheza mchezo wa kujihami dakika zote za mchezo waliwashangaza mashabiki wa Cameroon licha ya kufungwa kishujaa mabao 2-1 kutoka kwa wenyeji hao wa Afrika Magharibi.

Vijana hao wa Marcio Maximo walicheza mchezo wa mashambulizi ya kushtukiza na kama si bao la dakika za lala salama la Samuel Eto’o huenda hadithi ingekuwa nyingine.

Mechi hiyo ya kusisimua ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia na Mataifa ya Afrika ilifanyika jana mjini Yaounde.

Mchezaji bora wa zamani wa Afrika mara tatu, Eto’o alifunga mabao mawili ambayo yalivuruga mipango ya Stars katika kampeni za kuwania kucheza fainali za Mataifa ya Afrika na Kombe la Dunia mwaka 2010.

Vijana wa Maximo walishuka uwanjani kwa nguvu nyingi na kumbukumbu ya suluhu waliyoipata wiki iliyopita jijini Dar es Salaam na ndio maana mpaka mapumziko walikuwa wamewamudu Cameroon kwa kutoruhusu bao lolote na kwenda suluhu.

Kona ya 15 iliyopigwa na Geremi Njitap dakika ya 66 na kumtoka kipa Ivo Mapunda ilimkuta Eto’o aliyeunganisha kwa shuti kali mbele ya mabeki wa Stars.

Hata hivyo, Stars haikukata tamaa badala yake iliendelea kufanya mashambulizi ya kushtukiza na dakika ya 79, Danny Mrwanda alisawazisha baada ya kuwazidi ujanja beki Rigobert Song na Henry Bikey kabla ya kumvuta kipa, Iddriss Kamen na kufunga kirahisi. Alipokea pasi ya kupenyeza ya Nizar Khalfan.

Cameroon iliyoonekana kutafuta bao kwa nguvu dakika zote walishindwa kuipenya ngome ya Stars iliyokuwa ikiongozwa na mabeki imara, Nadir Haroub Cannavaro na Salum Sued ambaye hata hivyo aliumia dakika za mwisho na nafasi yake kuchukuliwa na Kelvin Yondani.

Huku kila mmoja akiamini kuwa mechi hiyo ingemalizika kwa sare, Eto’o alifunga bao la pili katika dakika ya 90 baada ya kuizuia krosi kwa mkono na kuachia fataki kali ambalo lilijaa wavuni na kumwacha Mapunda akiwa hana la kufanya.

Cameroon ambao walipata kona zaidi ya ishirini walikosa mabao kadhaa mmojawapo ikiwa ni dakika ya 35 wakati Eto’o akiwa eneo la hatari aliachia fataki ambalo lilipaa.

Kiujumla Cameroon walicheza kwa presha zaidi mbele ya mashabiki wao na mipango yao mingi ilikuwa ikivurugwa na msitu wa mabeki wa Stars ambao muda mwingi walikuwa makini kuondoa hatari zote langoni mwao.

Stars nayo ilikosa bao la wazi dakika za mwisho baada ya Jerry Tegete aliyekuwa ameingia kuchukua nafasi ya Mrisho Ngassa kushindwa kuunganisha kwa umakini krosi ya Shadrack Nsajigwa.

Katika mchezo huo nahodha Henry Joseph na Ngassa walipewa kadi za njano huku mwamuzi kutoka Gambia akionekana kuipendelea Cameroon.

Kwa matokeo hayo, Cameroon ina pointi kumi na Stars imebakiwa na pointi zake mbili katika mechi nne na matumaini ya Watanzania yatajulikana leo wakati Cape Verde itakapocheza na Mauritius mjini Praia katika Kundi la Kwanza.

Katika hatua nyingine, pamoja na kupewa huduma nzuri wakiwa Dar es Salaam, Cameroon jana waliwafanyia vurugu wachezaji wa Stars kabla ya kuanza kwa mchezo huo.

Kama kawaida yake kocha wa viungo, Itamar Amourim aliingia uwanjani mapema na kupanga koni na mipira upande moja wa uwanja na kwenda kuifuata timu kwenye vyumba vya kubalishia nguo ili kuanza mazoezi mepesi.

La kushangaza ni kuwa wenyeji waliingia uwanjani na kuanza kutoa mipira na koni iliyoweka na Itamar jambo ambalo lilifanya wachezaji wa Stars walipoingia uwanjani kushindwa kufanya mazoezi kwani Cameroon walikuwa wamevamia upande huo, hivyo kuzua mtafaruku kidogo kabla ya kamishna wa mchezo kuingilia kati.

Wachezaji wa Stars walikataa kuondoka eneo hilo, lakini alipoulizwa mmoja wa viongozi wa soka wa Cameroon alisema wenyeji ndio walikuwa na haki ya kuchagua upande wa kufanya mazoezi na si wageni.

Stars:Ivo Mapunda, Shadrack Nsajingwa, Amir Maftah, Salum Sued/Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Bonny, Shaaban Nditi, Henry Joseph, Danny Mrwanda, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa/Jerry Tegete.

Katika mechi nyingine jana, Afrika Kusini ilitoka suluhu na Sierra Leone huku Algeria ikiifunga Gambia bao 1-0.

Zambia iliifunga Swaziland bao 1-0 na Libya ikapeleka mauaji kwa Lesotho kwa kuifunga mabao 4-0.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments