Tanzania waiombea ushindi Taifa Stars Cameroon

HAKUNA njia ya mkato kusonga mbele kwa Taifa Stars katika kampeni zake za kufika Afrika Kusini na Angola 2010 zaidi ya kushinda mchezo wa leo.

Katika soka inawezekana. Stars inarudiana na Cameroon, The Indomitable Lions katika mchezo utakaofanyika kwenye mji wa Yaounde, Cameroon kuanzia saa 12:00 kwa saa za Tanzania. TBC1 itaonyesha mpambano huo moja kwa moja kutoka Yaounde.

Stars iliyokwishapoteza pointi saba mpaka sasa baada ya sare ya 1-1 na Mauritius, kuchapwa bao 1-0 na Cape Verde na suluhu ya Cameroon, inahitaji kushinda mchezo huo ili kufufua matumaini ya timu hiyo kufika Afrika Kusini na Angola mwaka huo.

Mpaka sasa, Stars iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili katika kundi la kwanza linaloongozwa na Cameroon yenye pointi saba ikifuatiwa na Cape Verde yenye pointi sita wakati Mauritius ina pointi moja.

Mchezo wa leo utakuwa mgumu ikitioliwa maanani kuwa Stars inataka kujikwamua wakati Cameroon inataka kumaliza udhia wa suluhu ya Tanzania ambayo hawakuitarajia.

Katika soka lolote linaweza kutokea kama ambavyo Senegal ilipofunge mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia, Ufaransa bao 1-0. Pamoja na kwamba watakuwa nyumbani, Stars ina uwezo wa kuifunga Cameroon, kwa kutilia maanani kuwa soka ina hali tatu, kushinda, sare na pia kushindwa.

Kocha wa Stars, Marcio Maximo ambaye hatulii timu yake inapocheza, atalazimika kufanya kazi ya kubwa kama aliyofanya wiki iliyopita kwenye Uwanja Mkuu wa Tanzania jijini Dar es Salaam licha ya kuwa ulimalizika kwa suluhu.

Hata hivyo, katika mchezo wa leo, Maximo atawakosa Abdi Kassim, Babi, ambaye anasumbuliwa na malaria na matatizo ya nyama za paja pamoja na Athuman Idd ‘Chuji’ ambaye anasumbuliwa na malaria ingawa alifanya mazoezi ya mwisho kabla ya timu haijaondoka jana asubuhi.

Maximo anatarajia kuwaunganisha safu ya mbele, Danny Mrwanda na Mrisho Ngassa licha ya kuwa na wao walikuwa majeruhi kabla ya kupata nafuu na kuanza mazoezi.

Huku akiwa na mkataba wa mwaka mmoja mkononi, Maximo baada ya kuusoma mchezo wa kwanza, anatarajia kutumia staili kufanya mashambulizi ya kushtukiza baada ya kuwasoma vizuri mabeki wa Cameroon katika mchezo wa kwanza na kujihami zaidi.

Katika kiungo wanatarajiwa kuwepo Henry Joseph ambaye hakucheza mchezo wa kwanza kutokana na kuwa na kadi. Mara kadhaa Maximo amekuwa akitumia viungo wengi kwa ajili ya kupunguza kasi ya mashambulizi ya timu pinzani. Henry ataunganisha nguvu na Godfrey Bonny.

Safu ya ushambuliaji, anatarajiwa Nizar Khalfan atakayekuwa na kazi ya kupandisha mipira mbele itakayowakuta akina Danny Mrwanda na Mrisho Ngassa ambaye alikuwa akiwapa tabu mabeki wa Cameroon watakaokuwa wakiongozwa na nahodha wao, Rigobert Song.

Langoni anatarajiwa Ivo Mapunda atakayekuwa chini ya uangalizi wa ngome yake itakayojengwa na Salum Sued, Shadrack Nsajigwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Amir Maftah ambao watakuwa na kazi ya kuzuia mashambulizi ya Cameroon yakiongozwa na Samuel Eto’o.

Mbali na wachezaji hao, Maximo pia anaweza kumpanga Emmanuel Gabriel ambaye alisema kabla ya kuondoka kuwa inaweza kuwachanganya Wacameroon kwa kuwa hawakumuona katika mchezo wa kwanza pamoja Ulimboka Mwakingwe . Pia Shaaban Nditi anaweza kuwemo katika kusaidia kupandisha mipira.

Stars inatakiwa kucheza kwa umakini bila kuwaza wachezaji wenye majina makubwa kama Bikey Amougou, Rigobert Song, Alexandre Song na Stephen Mbia ambao watakuwa chini ya kocha wao, Otto Pfister ambaye baada ya kuwasili katika mchezo wa kwanza, alisema kuwa anaiheshimu Tanzania kwa kuwa haijui soka yake.

Umakini wa ngome, kushambulia kwa malengo, kunaweza kuipa Stars mabao ambayo yataiweka pazuri. Cameroon pamoja na kushika nafasi ya kwanza Afrika kwa ubora wa soka na nafasi ya 13, ni timu kama zilivyo nyingine na inafungika.

Sala za Watanzania leo ni kuiombea timu yetu ishinde. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Stars.

IMEANDIKWA NA MWANANCHI.

Posted under:  All Articles

Tags:  

Comments